
Na Mwandishi Wetu, JAB.
Wakati Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) ikiufungua rasmi mfumo wa usajili wa Waandishi wa Habari wa https://taihabari.go.tz ili kuomba kuthibitishwa na kupatiwa Kitambulisho cha Uandishi wa Habari (Press Cards) Mwenyekiti wa Bodi hiyo Ndg. Tido Mhando amewaonya wenye nia ya kutumia vyeti visivyo halali wakati wa kujaza taarifa zao.
Mhando alitoa tahadhali hiyo tarehe 19 Mei, 2025 wakati akizungumza na Wahariri na Waandishi wa Habari wa vyombo mbalimbali vya Habari katika ofisi za Bodi hiyo zilizopo Mtaa wa Jamhuri jijini Dar es Salaam.


“Ndugu zangu Waandishi wa Habari, Bodi hii itaanza kutoa ithibati kwa waandishi wa habari wote kupitia mtandao na kutoa vitambulisho vya kidijiitali (digital Press Card). Maombi ya ithibati Press Cards yatafanyika kupitia Mfumo unaoitwa TAI-Habari”, alisema.
Mhando alisema mahitaji muhimu wakati wa kujaza taarifa katika mfumo huo kuwa ni pamoja na namba ya simu na barua pepe vinavyofanya kazi, picha ndogo (passport size) iliyoskaniwa barua ya utambulisho kutoka taasisi anayotoka au anakopeleka kazi zake ikiwa ni mwandishi wa kujitegemea (Freelancer), nakala ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA) na ada ya ithibati shilingi Elfu Hamsini (50,000).


“Mahitaji mengine ni vyeti vya elimu vilivyoskaniwa kwa mfumo wa PDF na kuthibitishwa na Mamlaka husika (kama chuo kikuu vithibitishwe na TCU na kama ni vyuo vya kati vithibitishwe na NACTVET), na katika hili nisisitize tafadhali sana usiweke cheti ‘feki’ jambo hilo linakiuka siyo tu linakiuka maadili ya taaluma habari, bali pia ni makosa yanatakayodhibitiwa kwa mujibu wa Sheria za nchi,” alisema Mhando.
Mhando alisema mahitaji hayo ni muhimu ili kukamilisha mchakato wa maombi kwa mafanikio na kwamba ni hatua inayolenga kuboresha huduma, kuimarisha usimamizi wa taaluma ya Uandishi wa Habari na kurahisisha upatikanaji wa vitambulisho kwa waandishi waliothibitishwa.
Aliomba Wahariri, Waandishi na wadau wote wakiwemo waajiri kutambua umuhimu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari katika kuimarisha weledi, maadili, na uwajibikaji wa taaluma ya uandishi wa habari nchini, na hivyo watoe ushirikiano wa hali ya juu katika kukuza na kuendeleza taaluma hiyo muhimu kwa taifa.
.jpg)
Akijibu maswali ya waandishi wa Habari kuhusu watu walio kwenye tasnia bila kuwa na vyeti vya Elimu ya Uandishi wa Habari, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo Wakili Patrick Kipangula alisema Sheria ilitoa muda wa miaka mitano kwa watu waliokuwa hawana sifa ili wakasome na kutimiza vigezo vya kisheria.
Alisema baada ya muda huo kuisha Waziri aliongeza muda wa mwaka mmoja na kwamba tangu Waziri aongeze mwaka mmoja ni miaka miwili imeshapita na kufanya jumla ya miaka nane na hivyo hakutakuwa na muda wa nyongeza tena.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...