Wizara ya Mifugo na Uvuvi imezindua rasmi mradi wa mafunzo kwa wataalamu wa mstari wa mbele wa afya ya mifugo, yanayofanyika katika nchi nne: Tanzania, Botswana, Zambia na Malawi.


Akizungumza leo Mei 17, 2025 katika Chuo cha LITA, Kampasi ya Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Riziki Shemdoe, amesema kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwapa ujuzi wa kisasa vijana, hususan wahadhiri wa chuo hicho, ili waendane na hali halisi ya sekta ya ufugaji ndani na nje ya nchi.


Mafunzo haya yameandaliwa kupitia mradi wa EDVET unaosimamiwa na shirika la MIOUT, kwa kushirikiana na wataalamu kutoka nchi za Hungary, Finland na Slovakia.


Prof. Shemdoe ameongeza kuwa washiriki wa mafunzo haya ni pamoja na wataalamu kutoka halmashauri za wilaya, manispaa na majiji, pamoja na walimu na wanafunzi wa chuo husika.


Akizungumzia juhudi za serikali, Prof. Shemdoe amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeanzisha kampeni kubwa ya chanjo kwa ajili ya magonjwa 13 sugu ya mifugo ambayo bado hayajatokomezwa. Kwa mwaka huu, kampeni hiyo itaanza na magonjwa matatu, ambapo ng’ombe milioni 19, mbuzi na kondoo milioni 17, pamoja na kuku milioni 40 wanatarajiwa kuchanjwa nchi nzima.


Amebainisha kuwa kampeni hiyo itaambatana na mpango wa utambuzi wa mifugo kwa kuweka hereni kwa ng’ombe, mbuzi, kondoo na kuku ili iwe rahisi kujua waliopata chanjo na mahali walipo.


“Hii itamsaidia mfugaji kwenye ufuatiliaji wa afya ya mifugo wake na pia kufungua fursa katika masoko ya kimataifa,” amesema Prof. Shemdoe.


Kwa upande wake, Dkt. Pius Mwambene, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mafunzo ya Mifugo (LITA), amesema kuwa baadhi ya wakufunzi watapatiwa mafunzo ndani ya nchi, huku wengine wakipewa fursa ya kwenda Hungary, Slovakia na Ubelgiji kwa ajili ya mafunzo ya juu ya utaalamu katika maeneo yanayohusiana na afya ya mifugo.


Ameongeza kuwa baada ya kukamilika kwa miaka miwili ya utekelezaji wa mradi huo, wakufunzi wote watakuwa wamepata mafunzo ya kisasa ambayo yatawawezesha kutoa huduma bora katika halmashauri zao kama wataalamu waliobobea, na hivyo kuchangia maendeleo ya sekta ya mifugo.




Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...