Dar es Salaam, Mei 2025 – Mitaa ya jiji la Dar es Salaam ilifurika shamrashamra Jumapili hii baada ya zaidi ya washiriki 3,500 kushiriki katika mbio ambazo sasa zimekuwa tukio maarufu la jiji – Absa Dar City Marathon 2025. Idadi hii imepanda kutoka washiriki 2,500 mwaka jana, ishara tosha kuwa mashindano haya yameendelea kuvutia umma na kuchangia katika michezo, jamii na sekta ya utalii nchini.
Mbio hizi ambazo huandaliwa na The Runners Club kwa udhamini
mkubwa wa Benki ya Absa Tanzania, sasa zimejikita kama tukio la kila mwaka la
mbio katikati ya jiji – zikiwa na ndoto ya kuwa tukio kubwa zaidi la riadha
siyo tu Tanzania bali pia Afrika Mashariki. Washiriki walichuana katika viwango
vitatu: kilomita 5, kilomita 10 na nusu marathon ya kilomita 21, huku mipango
ikiendelea kupanua zaidi tukio hili.
Mbio hizi ni zaidi ya ufanisi wa kiufundi wa wanariadha.
Kiini chake ni kukuza afya, mazoezi, mshikamano wa jamii na uzalendo wa
kitaifa. Akizungumza baada ya tukio, Beda Biswalo, Meneja wa chapa na
Mawasiliano wa Benki ya Absa Tanzania alieleza kuwa mbio hizi zinaendana na
lengo lao la kuhamasisha maisha yenye afya, kukuza mwingiliano wa kijamii na
kuchangia maendeleo ya jamii.
“Kwetu Absa, tunaamini kuwa Hadithi yako ni Muhimu. Huu siyo
msemo tu – bali ni dhamira yetu ya kutembea bega kwa bega na Watanzania wanapoandika
sura mpya zenye hamasa katika maisha yao. Afya bora ni msingi wa maisha yenye
maana, na marathon hii ni sehemu yetu ya kusaidia maelfu kuanza au kuendeleza
safari hiyo,” alisema Aron Luhanga, Mkuu wa Masoko na Mawasiliano ya Shirika wa
Absa Bank Tanzania.
Tukio hili limekuwa fursa muhimu kwa wakazi wa Dar es Salaam
kupumzika kutoka shughuli zao za kila siku na kuungana – iwe ni kushindana,
kushangilia au kuwasiliana kijamii. Vilevile, linamuunga mkono Mheshimiwa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika jitihada
zake za kuitangaza Tanzania kama kivutio cha utalii. Washiriki kutoka nje ya
nchi wanatarajiwa kuongezeka katika matoleo yajayo, hivyo kuiweka Dar es Salaam
kwenye ramani ya dunia ya mashindano ya mbio.
Kwa kuendeleza lengo la kusaidia jamii, sehemu ya ada za usajili wa mwaka huu itaelekezwa kusaidia wodi ya wazazi katika Hospitali ya Mnazi Mmoja. Aidha, kama sehemu ya shughuli za baada ya mbio, Absa inapanga kuendesha zoezi la uchangiaji damu kwa ajili ya benki ya damu ya taifa – jambo linaloonyesha wazi dhamira ya mashindano haya kutoa mchango kwa jiji na wakazi wake
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...