Mkuu wa Wilaya ya Songea Wilman Kapenjama Ndile, ametoa wito kwa wananchi na wadau wa sekta ya nishati kuhamasisha na kutumia nishati safi ya kupikia, akibainisha kuwa matumizi ya kuni na mkaa ni tishio kwa mazingira na afya ya jamii.
Akizungumza tarehe 10 Juni 2025 mjini Songea katika kikao cha wadau wa sekta ya mafuta kilichoandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, DC Ndile alieleza kuwa ni wakati muafaka kwa jamii kuachana na nishati chafu na kuchangamkia matumizi ya gesi, umeme na nishati mbadala kwa ajili ya kupikia.
Akiweka mkazo kwenye umuhimu wa nishati safi, alitoa mfano wa mafanikio ya Gereza la Mahabusu Songea ambalo awali lilitumia tani 40 za kuni kwa mwezi kupikia chakula cha wafungwa 200, lakini sasa linatumia vumbi la makaa ya mawe na matumizi yameshuka hadi tani 1 pekee kwa mwezi. Alisema mabadiliko hayo ni ushahidi kuwa matumizi ya nishati mbadala yanaweza kupunguza gharama, kulinda mazingira na kuboresha afya.
“Ukataji wa miti hovyo kwa ajili ya kuni na mkaa unachangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi. Tunapaswa kuchukua hatua sasa kwa kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala, salama na rafiki kwa mazingira,” alisema Ndile.
Kwa upande wake, Meneja wa EWURA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Karim S. Ally, alisisitiza kuwa mabadiliko ya kweli katika sekta ya nishati yanahitaji ushirikiano wa karibu kati ya mamlaka, wawekezaji na wananchi. Alibainisha kuwa mtu yeyote anayetaka kuuza au kusambaza gesi ya kupikia ni lazima apate leseni rasmi na kuzingatia masharti yaliyowekwa kwa usalama na ubora wa huduma.
Wadau waliohudhuria kikao hicho waliipongeza EWURA kwa juhudi zake katika kutoa elimu kuhusu usalama wa nishati na fursa zilizopo kwa wawekezaji, hasa katika kuanzisha vituo vya kusambaza gesi na mafuta vijijini, ambako bado kuna uhitaji mkubwa wa nishati mbadala.
Viongozi wa mitaa waliahidi kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya matumizi ya kuni na mkaa, huku wakihamasisha jamii kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.
Kwa sasa, Mkoa wa Ruvuma una jumla ya vituo vya mafuta 65, lakini bado kuna uhitaji mkubwa wa vituo vya nishati vijijini. Serikali na EWURA zimeendelea kutoa wito kwa wawekezaji kuwekeza zaidi katika maeneo haya ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora, salama na endelevu kwa wote.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...