Na Jane Edward, Arusha
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko, amefungua rasmi maonesho ya Karibu Kili-Fair yanayofanyika katika viwanja vya Magereza - Kisongo, jijini Arusha.
Dkt. Biteko amesema sekta ya utalii ni mhimili muhimu wa uchumi wa taifa kwani inachangia asilimia 7.9 ya pato la taifa na pia ni njia madhubuti ya kuitangaza Tanzania kimataifa.
Amesema kuwa Serikali inaendelea kutekeleza programu mbalimbali kama Royal Tour zinazolenga kuimarisha na kutangaza sekta ya utalii duniani kote kutokana na mchango wake mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi huku akiipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na waandaaji na washiriki wa maonesho ya Karibu Kili-Fair kwa juhudi zao katika kukuza sekta ya utalii.
Aidha, Dkt. Biteko ametoa maelekezo kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kuandaa mikakati ya kuendeleza mazao ya utalii yenye tija, pamoja na kutumia teknolojia ya TEHAMA katika kuitangaza Tanzania kimataifa na kusisitiza umuhimu wa kutumia ubunifu na teknolojia ili kuongeza ushindani wa kibiashara kwenye soko la kimataifa.
Vilevile, ametoa wito kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuendelea kuwekeza katika sekta ya utalii huku akiahidi kuwa Serikali itaendelea kuondoa vikwazo vinavyokwamisha maendeleo ya sekta hiyo na kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Makonda, ameiomba Wizara ya Maliasili na Utalii kulitambua eneo la Magereza - Kisongo kama eneo maalum kwa ajili ya maonesho ya kimataifa ya utalii ili kuvutia wageni kutoka mataifa mbalimbali.
Pia ameshauri muda wa maonesho hayo uongezwe kutoka siku 3 hadi siku 5 au 7 ili kutoa fursa zaidi kwa wawekezaji kuonesha bidhaa na huduma zao, hasa zinazohusiana na mnyororo wa thamani katika sekta ya utalii.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...