Farida Mangube, Morogoro
Wakati serikali ikiendeleza mapambano dhidi ya magonjwa hatarishi kwa afya ya binadamu, sekta ya kilimo nayo inakumbwa na changamoto ya ugonjwa wa Fungashada unaoathiri migomba na kutishia uwepo wa zao la ndizi nchini.
Ugonjwa wa Fungashada kitaalamu ukijulikana kama Banana Bunchy Top Disease (BBTD) unaosababishwa na virusi vya Banana Bunchy Top Virus (BBTV).
Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2022/2023, zaidi ya tani milioni 3.5 za ndizi zilivunwa nchini, huku karibu asilimia 60 zikizalishwa na wakulima wadogo, hususan katika mikoa ya Kagera, Kilimanjaro na Mbeya.
Akizungumza katika semina ya mafunzo kwa wakulima na maafisa kilimo iliyoandaliwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Afisa Kilimo Mkuu kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Hamad Lyimo alisema kuwa tangu kugunduliwa kwa mara ya kwanza Disemba 2020 wilayani Buhigwe, Kigoma, ugonjwa huo umesambaa hadi mikoa 11, ikiwemo Morogoro, Mbeya, Songwe, Mwanza, Dodoma, Katavi na Dar es Salaam.
“Mwaka 2024 wataalamu walithibitisha kuwa ugonjwa huu umevamia karibu kila kona ya mikoa inayozalisha ndizi kwa wingi, isipokuwa Kagera na Mara,” alisema Lyimo.
Dalili za Fungashada ni pamoja na mistari ya kijani (“J hooks”) kwenye majani, majani kunyauka kuanzia pembezoni kuelekea katikati, migomba kuwa mifupi na membamba kama shada la maua, na michirizi ya kijani kwenye ubavu wa majani. Ugonjwa huu haumwui mgomba mara moja bali humweka hai kwa muda mrefu, na hivyo kuwa msambazaji kimya wa virusi kwa migomba mingine.
Wataalamu wa kilimo wanakadiria kuwa BBTV unaweza kusababisha upungufu wa uzalishaji wa ndizi kwa zaidi ya asilimia 90, jambo ambalo linaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa mapato ya wakulima, viwanda vya usindikaji wa ndizi, masoko ya ndani na nje, na hatimaye usalama wa chakula kitaifa.
Aina maarufu za ndizi kama Mshale, Malindi, Bukoba na Kimalindi ziko hatarini kutoweka kabisa.
Binadamu ndio chanzo cha maambukizi.
Tofauti na magonjwa mengine ya mimea yanayosababishwa na wadudu au hali ya hewa, Fungashada husambazwa kwa kasi zaidi na binadamu kupitia uhamishaji wa miche ya migomba bila uchunguzi wala tahadhari.
“Bila kuondoa kabisa migomba iliyoathirika na kupanda miche salama kutoka kwa wazalishaji waliothibitishwa, ugonjwa huu utabaki kuwa tatizo kubwa,” alisema Dkt. Mpoki Shimwela, mtafiti wa migomba kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo TARI Maruku.
Dkt. Shimwela alibainisha kuwa kwa sasa mahitaji ya miche salama ya migomba ni makubwa mno, akitolea mfano Mkoa wa Kigoma ambao unahitaji miche milioni 4 kufidia athari za ugonjwa huo. “Serikali tayari imejenga maabara itakayozalisha hadi miche milioni 5 kwa mwaka, lakini bado haitoshi,” alisema.
Changamoto ya uzalishaji wa mbegu bora.
Hemadi Msofe, mchambuzi wa mbegu na mtaalamu kutoka TOSCI, alisema kuwa uzalishaji wa mbegu bora za migomba bado uko chini kutokana na ukosefu wa wazalishaji wa kutosha na rasilimali. “TOSCI ilianza kuandaa viwango tangu mwaka 2020 kwa kushirikiana na wadau ili kuhakikisha mbegu bora zinapatikana,” alifafanua.
Filbert Luhunga kutoka COSTECH aliwahimiza wakulima kutumia taarifa za kisayansi kufanya maamuzi sahihi, huku akionya dhidi ya matumizi ya miche isiyothibitishwa ambayo ndiyo chimbuko la maambukizi mapya.
Wito wa kuitangaza kuwa janga la kitaifa
Wataalamu wa kilimo na wadau mbalimbali wametoa wito kwa serikali kulitangaza rasmi Fungashada kama janga la kitaifa. Hii itawezesha kutengwa kwa bajeti maalum, kuongezwa kwa mafunzo kwa wakaguzi, kuanzishwa kwa mashamba ya mfano ya migomba salama, na kuongeza uelewa kwa wananchi.
“Tunaendelea kutegemea misaada kutoka kwa wafadhili kama USAID. Hatujaitangaza BBTV kama janga la kitaifa, na huo ni udhaifu mkubwa wa kimkakati,” alisema mtaalamu mmoja kutoka TPHPA kwa sharti la kutotajwa jina.
Godfrey Amba, mkulima kutoka Kata ya Kauzeni, Manispaa ya Morogoro, alisema kuwa upatikanaji mdogo wa miche bora ndio chanzo kikuu cha kuenea kwa magonjwa kama Fungashada. “Tunahitaji msaada wa haraka kutoka serikalini ili kulinda zao hili muhimu,” alisema.
Kwa sasa, kila mgomba unaoambukizwa ni sahani ya chakula inayopotea, kipato kinachofifia, na familia inayosogea karibu zaidi na umaskini. Hatua za haraka na za kisayansi zinahitajika kabla hali haijawa mbaya zaidi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...