Songea-Ruvuma.

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limesisitiza kuwa kila Mtanzania ni mnufaika wa huduma ya umeme iwe ni mteja wa moja kwa moja au la, kutokana na mchango wa huduma hiyo katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.

Akizungumza wakati wa ziara yake katika kata za Litisha na Liganga, Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Afisa Usalama Mkuu Msaidizi kutoka TANESCO Makao Makuu, Shami Yisuph Dunia, alieleza kuwa hata kama mtu hana huduma ya umeme nyumbani kwake, bado anaweza kufaidika kwa njia nyingine kupitia matumizi ya umeme kwenye saluni, mashine za kusaga nafaka, maduka, na huduma nyingine za kijamii zinazotumia nishati hiyo.

“Umeme unamgusa kila mmoja wetu, sio wateja wa TANESCO pekee. Kwa hiyo ni wajibu wa kila Mtanzania kuilinda miundombinu ya umeme kwa manufaa ya wote,”

Aliwahimiza wananchi kutumia umeme kwa uangalifu na kuacha tabia ya kuacha vifaa vya umeme vikiwa “on” pasipo matumizi, akisema hatua hiyo itapunguza gharama na kuimarisha huduma hiyo muhimu.

Aidha, Dunia alitoa onyo kali kwa watu wanaojaribu kupata huduma ya umeme kwa njia za mkato zisizo rasmi. “Haraka haraka haina baraka. Acheni kudanganywa na watu wanaojifanya wanaweza kuwasaidia kupata umeme haramu. Hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wahusika wote,”

Amesisitiza kuwa wahujumu wa miundombinu ya umeme mara nyingi si watu wa mbali, bali ni watu wa karibu watoto au ndugu zao, ametoa wito kwa jamii kushirikiana na TANESCO kuwadhibiti waharibifu wa miundombinu hiyo muhimu.

Naye Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja TANESCO Mkoa wa Ruvuma, Alan Njiro, alisema kuwa hakuna bei mbadala ya umeme zaidi ya iliyowekwa ni shilingi elfu 27 kwa maeneo ya vijijini.

“Maswali yote kuhusu huduma ya umeme, wasisite kuwasiliana moja kwa moja na TANESCO. Msikubali kupotoshwa na watu binafsi,” alisema Njiro.

TANESCO imetoa rai kwa wananchi kuwatambua na kuwaangalia kwa makini watu wanaojitambulisha kuwa ni watumishi wa shirika hilo, ili kuepuka udanganyifu na uharibifu wa miundombinu.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...