Denis Mguye, Afisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa wa Arusha na Mratibu wa Malezi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (ECD), ameona mabadiliko makubwa yakichukua nafasi—mabadiliko yanayobadilisha familia na mustakabali wa jamii katika Mkoa wa Arusha.

“Wanaume sasa wanasimama bega kwa bega na wake zao kliniki—jambo ambalo halikuwazwa kutokea hata miaka michache iliyopita,” anasema.

Ni nini kimechochea mabadiliko haya? Mzazi Hodari, mpango wa miaka miwili wa kipekee unaomaanisha "mzazi bingwa", umewezesha serikali za mitaa, watoa huduma za afya na familia kufafanua upya malezi yenye uwajibikaji, wakigeuza maono kuwa vitendo.

Kwa mara ya kwanza, baadhi ya mamlaka za serikali za mitaa katika Mkoa wa Arusha zinaandaa kujumuisha mikakati ya malezi ya awali ya watoto katika bajeti zao rasmi kuanzia mwaka ujao wa fedha.

Hii ni zaidi ya mabadiliko ya sera—ni ishara ya kujitolea kwa kina.

“Hii si tu kufuata maelekezo,” anasema Mguye. “Ni kutambua kuwa malezi na maendeleo ya mtoto ni kiini cha ustawi wa mkoa.”

Mtazamo huu mpya wa mkoa unalingana na kanuni za Mwongozo wa Uendeshaji na Uwasilishaji wa Mipango ya Ustawi wa Jamii katika Halmashauri (CCSWOPG) uliozinduliwa mwaka 2022, wenye lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya serikali, wadau, na jamii katika maeneo muhimu ya ustawi wa kijamii, ikiwemo ECD.

Wakati mipango ya awali kama Malezi III iliweka misingi muhimu, timu ya ECD ya Arusha ilitambua kuwa uhamasishaji wa vitendo unaotoka kwa jamii wenyewe ulikuwa muhimu.

Hapo ndipo Mzazi Hodari ulipojitokeza kuwa tofauti. Kupitia mfano wa mtu kwa mtu, ujumbe wa karibu na rasilimali zinazoeleweka, uliwagusa wanajamii moja kwa moja.

“Tumeona kwa macho yetu jinsi mbinu hii inavyowapa wazazi uwezo wa kuleta mabadiliko wao wenyewe,” anasema Mguye. “Sio wataalamu tu wanaozungumza—ni majirani, marafiki na wenzao wakisaidiana.”

Violet Chahe, Mratibu Msaidizi wa Afya ya Uzazi na Mtoto katika Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, anasimulia mabadiliko ya mtazamo.

“Sasa tunawaona baba, waliokuwa wamefungwa na mila, si tu kuhudhuria kliniki na wake zao bali pia kucheza na watoto na kushiriki katika malezi nyumbani. Mabadiliko haya, yaliyochochewa na Mzazi Hodari, yanaimarisha familia na kutuhamasisha kupanua afua wilaya nzima.”

Moja ya matokeo yasiyotarajiwa? Waandishi wa habari kuwa mabalozi wa malezi. Kilichoanza kama vipindi vya redio kwenye kituo kimoja kimekua hadi kuwa harakati; sasa vikifikia vituo sita vya redio za jamii, ambapo waandishi wa habari wanaongoza mijadala ya malezi, wakialika wataalamu na kuunda mwelekeo wa mjadala wa umma.

Wengi wameenda zaidi ya kuripoti—wamekuwa mabingwa wa malezi bora wao wenyewe. Mguye anasimulia hadithi za baba waliovutiwa na matangazo haya au kushawishiwa na wake zao kuanza kushiriki. Hata katika maeneo ambayo Mzazi Hodari haujafika rasmi, athari zake zinaonekana zikithibitisha jinsi mazungumzo halisi ya kijamii yanavyosambaa kwa mbali.

Harakati hii imeleta mabadiliko hadi ngazi ya uongozi wa mkoa, ikiathiri sera, vipaumbele, na mtazamo wa jamii kuhusu malezi.

Timu maalum ya mabingwa wa ECD imeibuka katika Sekretarieti ya Mkoa wa Arusha. Baadhi wanatumia maarifa hayo majumbani kwao, na wengine wanaomba vipindi vya malezi kwenye kata wanazozisimamia.

“Ni ule uhalisia wa mbinu ndio unaifanya iwe na nguvu,” anasema Mguye. “Imetengenezwa kwa kuzingatia jamii zetu—ni ya vitendo, yenye heshima, na rahisi kuitumia.”

Zaidi ya vikao rasmi, mazungumzo yanabadilika hata katika maeneo ya kawaida. Makundi ya WhatsApp,yaliyokuwa yakijaa gumzo za kila siku kati ya waendesha bodaboda, wauzaji madukani na wakulima sasa yana mijadala ya lishe, usalama wa watoto, na msaada wa kihisia, yakibadilisha mazungumzo ya kawaida kuwa fursa za kujifunza na kuleta mabadiliko.

Mguye anazungumzia Kinara mmoja wa kiume kutoka jamii ya kimila ambaye awali alichekwa kwa kushiriki katika malezi:

“Watu walimcheka,” anasema Mguye. “Lakini walipoona mabadiliko halisi—watoto wenye afya bora, migogoro michache—walimpa heshima. Leo hii, ni sauti inayoaminika katika jamii yake.”

Kliniki za maeneo mbalimbali nazo zimeona athari.

Familia zinakuja pamoja, wanauliza maswali zaidi, na hufuata maendeleo ya watoto wao kwa karibu. Viashiria vya maendeleo ya awali ya mtoto kwenye kadi za afya vinafikiwa kwa kiwango cha juu zaidi. Wazo kwamba malezi ni jukumu la pamoja halijajulikana tu—limekubalika.

“Mzazi Hodari imeleta mazungumzo kuhusu malezi na mshikamano katika maeneo ambapo hayakuwepo,” anasema Mguye. “Umefanya watu waamini kuwa wanaweza kufanya mambo kwa njia tofauti—na bora zaidi.”

Akielezea mafanikio haya, Mguye anaona taswira ya siku zijazo ambapo mikutano ya robo mwaka italeta pamoja vinara ili kuchambua takwimu, kushiriki hadithi kutoka mashinani, na kupanua mbinu bora katika mkoa wote. Pia anaona fursa za ubunifu katika uhamasishaji, kama vile michezo ya soka ya jamii yenye maudhui ya malezi na maendeleo ya awali ya watoto.

“Hizi ni dalili za mwanzo tu,” anasema. “Lakini kizazi kijacho kitaona matokeo halisi—vijana watakaokua wakiwa na misingi imara, familia zenye afya, na hali ya kujiamini. Hicho ndicho kizazi tunachokilea.”

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...