Madereva wa magari ya serikali pamoja na taasisi za umma Mkoani Songwe wamekumbushwa kuwa na nidhamu na kuongea na barabarani kwa kuzingatia sheria za usalama barabarani ikiwa ni pamoja na kuwa wa shauri wa viongozi wanaowaendesha juu ya masuala ya usalama barabarani ili kupunguza ajali zinazoweza kuepukika ikiwa ni pamoja na kulinda usalama wa watumiaji wengine wa barabara.

Rai hiyo imetolewa Juni 01, 2025 na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Songwe Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Charles Bukombe wakati wa Semina ya utoaji wa elimu ya usalama barabarani kwa madereva hao katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe.

Katika Semina hiyo, SSP Bukombe alieleza na kufafanua wajibu wa dereva ambao ni kufuata sheria, alama na michoro ya barabarani ili kuwa salama katika majukumu yao ya kila siku. Pia aliwataka madereva hao kujiendeleza kusoma juu ya taaluma yao kutokana na mabadiliko ya teknolojia ambayo inawataka kujipanga wakati na baada ya maisha ya kazi kwa mstakabali wa maisha yao baada ya kazi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Mbozi Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Anton Sabasaba amesema kuwa katika semina hiyo walijikita zaidi kuwaelimisha madereva hao juu ya madhara ya mwendokasi, kuvipita vyombo vingine sehemu ambazo haziruhusiwi ikiwa ni pamoja na kuchukuwa taadhari sehemu ambazo ni makazi ya watu ili kuepusha ajali zinazoweza kuepukika.

Vilevile katika Semina hiyo, madereva hao walipata wasaa wa kukumbushwa sheria mbalimbali za usalama barabarani na Koplo Chika Sanda pamoja na Koplo Maganga Kalulumya kutoka Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Songwe na kuwataka kuwa na kitabu cha sheria hizo ili kujikumbusha kwa lengo la kuendelea kuwa salama kipindi chote cha utendaji wa majukumu yao ya kila siku pamoja na watumiaji wa barabara.

Kwa niaba ya madereva wengine baada ya kupewa nafasi ya kuuliza maswali, maoni, ushauri na changamoto zinazowakabili, Bw. Fungafunga Njovu ambaye ni dereva kutoka Halimashauri ya Mji wa Tunduma alitumia nafasi hiyo kulishukuru Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe kwa elimu waliyoipata na ameomba mafunzo hayo yawe endelevu ili kuendelea kuwajengea uelewa juu ya umuhimu wa sheria za usalama barabarani na ameahidi kushirikiana na Jeshi la Polisi hasa katika masuala ya usalama barabarani.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...