Na Seif Mangwangi, Arusha

RAIA wa nchi ya Mali Jaji Modibo Sacko amechaguliwa kuwa Rais mpya wa Mahakama ya Kimataifa ya Watu na Haki za Binaadam (AfCPHR), akichukua nafasi ya Mtanzania Jaji Imani Aboud.

Jaji Aboud amehudumu nafasi hiyo kwa vipindi viwili huku Rais mpya anayechukua nafasi yake akihudumu kama makamu wa Rais wa Mahakama hiyo katika kipindi cha pili cha uongozi wa Jaji Aboud.

Katika uchaguzi huo uliofanyika juzi, nafasi ya Makamu wa Rais amechaguliwa Jaji Bensaoula Chafika kutoka Algeria.

Akizungumza na waandishi wa habari, Rais mpya Jaji Modibo ameishukuru Tanzania kwa uamuzi wake wa kuendelea kuhudumia mahakama hiyo.

Pia amemshukuru Rais anayemaliza muda wake Jaji Aboud akimuelezea kuwa amekuwa msaada mkubwa kwake kama kiongozi wa mahakama hiyo na kama msaidizi wake katika nafasi ya makamu wa Rais wa Mahakama hiyo

Amesema katika uongozi wake ataendeleza mambo aliyoyaacha mtangulizi wake Jaji amani Aboud na kusisitiza utekelezwaji wa maamuzi yanayotolewa na mahakama hiyo.

Kwa upande wake Rais anaemaliza muda wake Jaji Imani Aboud, ameeleza kuhusu mafanikio yaliyopatikana pamoja na changamoto zinazoikabili Mahakama hiyo, hasa kutotekelezwa kwa maamuzi yake na baadhi ya nchi wanachama wa Umoja wa Afrika.

" Mahakama imekuwa ikitoa maamuzi lakini nchi wanachama wamekuwa hawatekelezi maamuzi hayo, hili sio lengo la kuanzishwa kwa mahakama hii, tungependa ifikie mahali maamuzi tunayopitisha basi yafanyiwe kazi,"amesema

Amesema Mahakama hiyo haina mamlaka ya moja kwa moja ya kuhakikisha utekelezaji wa hukumu zake jambo ambalo linahitaji juhudi za pamoja kutoka kwa vyombo vingine vya Umoja wa Afrika, hasa Baraza la Mawaziri wa Mambo ya Nje.

“Hii si changamoto ya Mahakama yetu pekee, bali ni changamoto ya Mahakama nyingi za Afrika na hata za kimataifa,” alieleza Jaji Aboud.

“Tunaendelea na mazungumzo na viongozi wa Umoja wa Afrika ili kuboresha utekelezaji wa maamuzi ya Mahakama hii kwa manufaa ya wananchi wa Afrika.”

Akiangazia mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wake Jaji Aboud alieleza kuwa Mahakama hiyo imepata ushirikiano mkubwa kutoka kwa serikali mbalimbali na kufahamika si tu barani Afrika bali pia kimataifa.

Aidha, alitaja mafanikio kama kufanikisha ujenzi wa jengo la kudumu la Mahakama hiyo ambalo limekuwa katika mipango kwa zaidi ya miaka 20 na sasa liko tayari kuzinduliwa ndani ya miezi michache ijayo.
Rais Mpya wa Mahakama ya Kimataifa ya Afrika  ya Watu na Haki za Binaadam, Jaji Modibo Sacko Raia wa Mali
Makamu mpya wa Rais wa Mahakama ya Kimataifa ya Afrika ya Watu na Haki za binaadam Raia wa Algeria Jaji,Bensaoula Chafika

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...