Na. MWANDISHI WETU – GENEVA USWIZI

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Duniani (World Meteorological Organization - WMO) Bi. Celeste Saulo ameahidi kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha mfumo wa Tahadhari ya mapema (early warning systems) kwa ajili ya kuchukua hatua za haraka kuzuia na kukabiliana na maafa pindi yanapotokea.

Ameyasema hayo wakati wa kikao cha pembezoni mwa Jukwaa la Nane la Dunia la Kupunguza Madhara ya Maafa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, na Uratibu, Dkt. Jim Yonazi pamoja na ujumbe alioongozana nao kwa lengo la kuzungumza mikakati na mipango ya kuendeleza ushirikiano mapema 05 Juni 2025 mjini Geneva Uswizi.

Bi. Celeste Saulo amesema wapo tayari kuwezesha maeneo mbalimbali ikiwemo ya kuongeza ueleza kupitia mafunzo kwa wataalam kwenye masuala ya Matumizi ya Taarifa za hali ya hewa pamoja na masuala muhimu kama elimu na kuona namna wanavyoweza kuunga nguvu za Pamoja katika matumizi ya vifaa vya kisasa vya utabiri wa hali ya hewa na matumizi ya taarifa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya hewa kwa lengo la kuendelea kuwa na tahadhari za mapema.

“Tunaendelea kushirikiana na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kwa kuwa tuna ushirikiano wa muda mrefu.Aidha, tunazingatia umuhimu wa kuimarisha usimamizi wa maafa kwa kuzingatia hatua zinazochukuliwa na Tanzania ya kujenga uwezo pamoja na kushirikiana na nchi zingine na kuandaa miradi ambayo inazingatia vipaumbele vyenye maslahi kwa wote,” alisisitiza Bi. Saulo

Kwa hatua hiyo Bi. Saulo ameipongeza Tanzania kwa namna imeendelea kuwa ya mfano katika kuratibu, masuala ya menejimenti ya maafa na kuhakikisha wanakuwa na mifumo ya tahadhari za mapema inayowasaidia katika kupeana taarifa za mapema zinazosaidia kuzuia madhara yanayoweza kutokea wakati wa maafa

Aidha alifafanua kuwa mifumo ya tahadhari za mapema ni muhimu kwani inasaidia kuandaa mifumo jumuishi ya kupeana taarifa za tahadhari za mapema; kupata taarifa mapema zinazosaidia kupunguza madhara ya majanga, kuwezesha upatikanaji wa taarifa za awali zitakazosaidia kuimarisha mfumo wa maisha ya jamii ambayo iko katika hatari ya kuathirika na majanga na kupunguza madhara katika kujiandaa kwa ajili ya maafa yanayoweza kutokea.

Katika mazungumzo hayo, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, na Uratibu, Dkt. Jim Yonazi amesisitiza dhamira ya Serikali ya Tanzania kuendeleza ushirikiano na Mamlaka ya Hali ya Hewa Duniani katika kuimarisha masuala ya usimamizi wa maafa inayolenga kuwawezesha kuwa na jamii stahimilivu na majanga na kuifanya Dunia kuwa sehemu salama ya kuishi.

Akiongelea namna Tanzania inavyoendelea kuratibu masuala ya Menejimenti ya maafa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo ili kuendela kulinda jamii isipatwe na madhara yatokanayo na maafa huku akiainishsa mafanikio makubwa ikiwemo la uwepo wa Kituo cha Ufuatiliaji wa Mwenendo wa Majanga na Tahadhari ya Mapema (National Emergency Operation and Communication Center Situation Room) katika Kituo cha Taifa cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura nchini Tanzania chenye tija kwa Taifa kwani kimerahisisha utekelezaji na utendaji wa haraka katika masuala ya maafa.

Viongozi hao wamejadili umuhimu wa kuweka mikakati madhubuti ya maendeleo jumuishi ili kuhakikisha juhudi za pamoja katika kukabiliana na maafa kwa kushirikiana na wadau wengine ili kuinufaisha jamii nzima.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi  akisalimiana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Duniani Bi. Celeste Saulo wakati walipokutana kwa ajili ya kikao cha pembezoni mwa Jukwaa la Nane la Dunia la Kupunguza Madhara ya Maafa na kufanya mazungumzo kuhusu mikakati na mipango ya kuendeleza ushirikiano katika masuala ya menejimenti ya maafa.Kikao hicho kimefanyika mjini Geneva Uswizi.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi  akieleza namna Tanzania ilivyopiga hatua katika masuala ya menejimenti ya maafa wakati wa kikao cha pembezoni mwa Jukwaa la Nane la Dunia la Kupunguza Madhara ya Maafa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Duniani (World Meteorological Organization - WMO) Bi. Celeste Saulo walipokutana kwa ajili ya kikao hicho kilichofanyika mjini Geneva Uswizi.
Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, na Uratibu) Brig. Jenerali Hosea Ndagala akichangia jambo wakati wa kikao cha pembezoni mwa Jukwaa la Nane la Dunia la Kupunguza Madhara ya Maafa kilichowakutanisha Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Duniani Bi. Celeste Saulo mjini Geneva Uswizi.

(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...