Na MWANDISHI WETU- CHALINZE

SERIKALI imesisitiza kuwa imejipanga kuhakikisha kuwa wafugaji nchini wanakuwa na uwezo wa kufanya ufugaji wa kisasa wenye tija zaidi na kuachana na mbinu duni kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa mifugo kutoka ndani na nje ya nchi.

Hayo yasemwa jana Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti, wakati wa uzinduzi wa Maonesho ya Tatu ya Mifugo ya Nchi Tatu 2025 yaliyofanyika katika Kijiji cha Ubena Zomozi, Halmashauri ya Chalinze, Wilaya ya Bagamoyo, ambapo maonesho hayo yamefadhiliwa na Benki ya NMB na kuandaliwa na Kampuni ya Mbogo Ranches, chini ya kaulimbiu: “Kujenga Ushirikiano, Kukuza Kilimo”.

Maonesho hayo yalihudhuriwa na wafugaji kutoka nchi tatu ambazo ni Tanzania, Kenya na Namibia, pamoja na Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Isaac Njenga na Kamishna Mkuu wa Namibia, Lebbius Thobias pamoja na waonyeshaji wa vifaa na bidhaa mbalimbali za kilimo kutoka kampuni mbalimbali.

“Asilimia takribani 97 ya ng’ombe nchini ni wa asili, ambao hutoa wastani wa kilo 80 hadi 120 za nyama kwa ng’ombe mmoja, na maziwa ni kati ya lita moja hadi tatu kwa siku kwa kila ng’ombe. Aina hii ya uzalishaji haina tija, ndiyo maana Serikali inashirikiana na wadau mbalimbali kuleta mapinduzi katika sekta hii,” alisema Mnyeti.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya ya Biashara Benki ya NMB, Msolo Mlozi alisema kuwa hadi sasa benki hiyo imetoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 100 kwa wafugaji nchini kwa madhumuni mbalimbali ikiwemo kunenepesha mifugo, kununua chakula bora cha mifugo, kununua aina bora za mifugo na kujenga miundombinu bora ili kuongeza uzalishaji.

“Benki yetu inafahamu changamoto zinazowakumba wafugaji kama vile uhaba wa chakula na maji hasa wakati wa kiangazi, magonjwa ya mifugo, uzalishaji mdogo kutoka kwa mifugo wa asili, na ukosefu wa makazi ya kudumu kwa wafugaji. Kupitia mikopo tunayotoa, wafugaji wanaweza kukuza au kununua chakula cha mifugo, kuchimba visima vya kudumu na kutatua tatizo la ukosefu wa maji, pia kuhudhuria mafunzo mbalimbali ya kuongeza maarifa,” alisema Mlozi

Naye Mkurugenzi wa Mbogo Ranches, Naweed Mulla alisema kuwa maonesho haya yameandaliwa kwa lengo la kuwawezesha wafugaji wa ndani kujifunza mbinu za kisasa kutoka kwa wenzao wa nchi jirani pamoja na kupata fursa ya kununua mifugo bora ya ng’ombe, mbuzi, kondoo na kuku ili kuongeza uzalishaji.

“Tukio hili ni fursa nzuri kwa wafugaji wetu kupata maarifa ya ufugaji wa kisasa na kuyatekeleza. Pia ni jukwaa nzuri kwa washiriki wa nchi zote tatu kuungana na kuendeleza mawasiliano,” alisema.

Kwa nyakati tofauti, Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Isaac Njenga na Kamishna Mkuu wa Namibia, Lebbius Thobias, walisisitiza umuhimu wa nchi hizo tatu kuongeza ushirikiano katika sekta ya mifugo ambayo walisema inatoa fursa nyingi za kiuchumi kwa watu binafsi na kwa taifa kwa ujumla.

“Wakati Rais wetu Dk. Netumbo Nandi Ndaitwah, alipotembelea nchi hii mwezi uliopita, alifanya mazungumzo na Rais Samia Suluhu Hassan, na moja ya mambo waliyoyajadili ni kukuza sekta ya mifugo. Tukio hili ni ishara tosha kuwa sekta ya mifugo inatambuliwa kwa mchango wake muhimu katika maisha yetu ya kila siku,” alisema.

Taiko Tarongei, mfugaji kutoka Ubena, Halmashauri ya Chalinze, alisema kuwa kupitia maonesho hayo amejifunza umuhimu wa kutumia mbinu za kisasa za ufugaji na ameahidi kuzitumia ili kuongeza tija.












Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...