Na Mwandishi Wetu,Michuzi TV

NAIBU Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Doto Mashaka Biteko, amesema kuna uhusiano mkubwa kati ya kilimo na lishe huku akisisitiza  kilimo chenye mwelekeo wa lishe kinaweza kupunguza utapiamlo na magonjwa yatokanayo na lishe duni.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati akifungua Wiki ya Mkutano wa Kilimo, Lishe na Afya (ANH2025) ambapo washiriki 1500 kutoka mataifa  50 duniani wameshiriki , Dk.Biteko amesema Serikali itaendelea kupambana na udumavu unaoathiri zaidi ya asilimia 30 ya watoto chini ya miaka mitano nchini.

Pia itadhibiti tatizo la uzito kupita kiasi na upungufu wa virutubishi kupitia Mpango wa Kitaifa wa Utekelezaji wa Lishe wa Sekta Mbalimbali. “Tanzania, kilimo kinachangia asilimia 29 ya Pato la Taifa na kuajiri zaidi ya asilimia 65 ya wananchi. 

“Ndiyo maana bajeti ya kilimo imeongezwa kwa asilimia 29. Serikali pia inaendelea kutekeleza programu mbalimbali kama vile ‘Jenga Kesho Iliyo Bora’ (BBT), inayowasaidia wakulima wadogo kupata pembejeo bora, zana za kilimo, miundombinu ya umwagiliaji na elimu ya ugani,” amesema Dkt. Biteko. 

Maboresho makubwa yamefanyika, ikiwemo ongezeko la asilimia 7 la vituo vya afya tangu 2021, ajira ya wahudumu wa afya ya jamii wapatao 137,000, pamoja na kupanua huduma za kidijitali ili kupambana na magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza.

Kwa upande wake Naibu Katibu Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia amesema kwamba alisema kupitia  elimu bora nchi inaweza kuongeza tija katika sekta za kilimo, afya na lishe.

Wakati huo huo Naye, Mwenyekiti wa Mkutano huo, Profesa Sunnetha Kadiyala kutoka Shule ya Lishe na Tiba ya Magonjwa ya Kitropiki ya London, ameeleza mkutano huo malengo yake ni  kuimarisha matumizi ya tafiti na sayansi katika sera kupanua wigo wa ushirikiano wa kimataifa.

Pia kuhakikisha vijana wanasayansi wanajengewa uwezo kupitia programu za mafunzo na ushauri. Alisisitiza umuhimu wa kuongeza kasi ya utafiti wa kisayansi ili kuboresha mifumo ya chakula, kupunguza njaa na kuhakikisha usalama wa chakula.

“Tanzania imekuwa mwenyeji wa Mkutano wa Kilimo, Lishe na Afya (ANH2025), ukijumuisha washiriki kutoka zaidi ya nchi 50 duniani. Mkutano huu umeandaliwa na ANH Academy kwa kushirikiana na Shule ya Lishe na Tiba ya Magonjwa ya Kitropiki ya London (LSHTM) pamoja na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo.”

Awali Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Prof. Raphael Chibunda, ameeleza SUA inajivunia kuwa mwenyeji mwenza wa mkutano huo, ambao unawaleta pamoja watafiti na watunga sera ili kuimarisha kilimo na lishe nchini. 

“Lengo kuu la mkutano huo ni kuangalia namna ya kuboresha kilimo chetu ili kitoe mazao yenye lishe bora, hivyo kupunguza magonjwa yanayosababishwa na ukosefu wa lishe.” Amesema na kusisitiza wadau wa kilimo na lishe wanaoshiriki mkutano huo watapata nafasi ya kujadiliana kwa kina kuhusu masuala yanayohusu lishe na kilimo.























 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...