WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema kuwa Serikali itaendelea kuwapa kipaumbele walimu nchini kutokana na nafasi yao muhimu katika maendeleo ya taifa na jamii kwa ujumla.

Prof. Mkenda alitoa kauli hiyo jana usiku wakati wa hafla ya utoaji wa zawadi kwa washindi wa shindano la tatu la stadi za ufundishaji kwa elimu ya msingi na shindano la kwanza kwa walimu wa elimu ya sekondari.

Amesema kuwa Serikali inapanga kuingiza bajeti ya shindano hilo katika mwaka wa fedha 2025/2026, kwa kuwa linaongeza hamasa na motisha kwa walimu wanaofundisha wanafunzi katika ngazi mbalimbali.

"Walimu ndio nguzo ya msingi ya elimu. Serikali itaendelea kuweka mkazo katika kuwawezesha na kuwathamini, kwa sababu wao ndio wanaowatengeneza wataalamu wa kesho," alisema Prof. Mkenda.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dkt. Aneth Komba, alisema kuwa shindano la mwaka huu limehusisha walimu wa sayansi kwa kidato cha kwanza kwa upande wa sekondari, huku likiwa ni mara ya tatu kufanyika kwa elimu ya msingi.

Ameeleza kuwa shindano hilo ni sehemu ya utekelezaji wa maboresho ya mtaala wa mwaka 2023, na linaongeza ujuzi wa walimu hasa katika matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), jambo ambalo ni muhimu kwa wanafunzi wa karne ya sasa.

Hata hivyo, Dkt. Komba alitaja changamoto ya baadhi ya walimu kurekodi maudhui yasiyofaa, akibainisha kuwa hilo ni eneo ambalo linahitaji kufanyiwa kazi ili kuboresha mashindano yajayo.

Akizungumza katika hafla hiyo, mwakilishi mkazi wa Benki ya Dunia, Gema John, ambaye ni mmoja wa wadhamini wakuu wa mashindano hayo, alisema benki hiyo imekuwa ikiwekeza katika sekta mbalimbali, ikiwemo elimu ya awali na sekondari.

"Tumeamua kushirikiana na TET kuwekeza kwa walimu kwa sababu tunaamini walimu bora ndio msingi wa elimu bora. Na mwaka huu tumeongeza ushiriki kwa walimu wa sekondari," alisema Gema.
















Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...