Dar es Salaam, Juni 21, 2025 — Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, amesema kuwa Kongamano la Kitaifa la Sheria ni jukwaa muhimu linalowawezesha wananchi kufahamu haki zao za msingi na kupata uelewa mpana wa Sheria za Uchaguzi.

Akifungua kongamano hilo leo jijini Dar es Salaam, Dkt. Kikwete amesema demokrasia ya Tanzania imepitia hatua mbalimbali tangu enzi za mfumo wa chama kimoja hadi kuingia kwenye mfumo wa vyama vingi vya siasa.

“Ni muhimu wananchi kuchambua kwa makini hoja za wanasiasa ili kuchagua viongozi bora watakaoiongoza nchi kwa weledi na uzalendo,” alisisitiza.

Amesema mabadiliko ya sheria mbalimbali yamefanyika katika vipindi tofauti, kuanzia Awamu ya Nne hadi ya Sita, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha Watanzania wanashiriki kikamilifu katika chaguzi za Rais, Wabunge na Madiwani.

Akizungumzia maboresho ya sheria za uchaguzi yaliyofanyika mwaka 2024, Dkt. Kikwete amesema moja ya mafanikio ni kuboreshwa kwa mfumo wa uteuzi wa wasimamizi wa uchaguzi ambao sasa unafanywa na Tume Huru ya Uchaguzi, hatua inayoongeza uwazi na kuimarisha uhuru wa uchaguzi nchini.

Aidha, alitoa rai kwa watu wanaopotosha kuhusu mabadiliko hayo kuacha mara moja, akibainisha kuwa baadhi ya vipengele kama suala la mgombea kupita bila kupingwa tayari vimefanyiwa marekebisho ili kuimarisha misingi ya demokrasia.

“Sheria nyingi sasa zimeandikwa kwa lugha ya Kiswahili ili kuwawezesha wananchi wengi kuzisoma, kuzifahamu na kuzitumia,” alisema Dkt. Kikwete.

Kwa upande wake, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Hamza Johari, alisema kongamano hilo ni la kwanza kufanyika tangu kuanzishwa kwa Chama cha Mawakili wa Serikali, kikilenga kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya kisheria yanayohusu uchaguzi mkuu ujao.

“Sisi ni mawakili wa Serikali na askari wa kalamu. Hili ni jukwaa mahsusi la kutoa elimu ya kisheria kwa wananchi ili kuwaongezea uelewa,” alisema Dkt. Johari.

Naye Rais wa Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania, Bavoo Junus, alisema kongamano hilo limelenga kuwajengea wananchi uelewa kuhusu sheria za uchaguzi na haki zao za kikatiba, hasa katika kipindi hiki ambapo Taifa linaelekea kwenye uchaguzi mkuu wa 2025.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...