* Filamu 430 zapokelewa kutoka Nchi za Afrika, Ulaya……

Na Leandra Gabriel, Michuzi TV

MAANDALIZI ya Tamasha la Kimataifa la Filamu la Zanzibar (ZIFF,) maarufu kama Tamasha la Nchi za Majahazi msimu wa 28 kwa mwaka 2025 yamekamilika na kuelezwa kuwa litafanyika Juni 25 hadi 29 mwaka huu Ngome Kongwe Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari leo  Katika ukumbi wa Goethe Institut jijini Dar es Salaam Mtendaji Mkuu wa ZIFF, Joseph Mwale amesema kuwa ; Maandalizi kwa ajili ya Tamasha hilo kwa mwaka huu yamekamilika na litabebwa na kauli mbiu ya ‘Tumaini Linalochipukia.’ 

Amesema Tamasha hilo ambalo limekuwa kivutio barani Afrika na duniani kwa ujumla limeendelea kuvutia watu wengi zaidi na kwa mwaka huu licha ya burudani mafunzo mbalimbali yanayohusu uandaaji wa filamu yatatolewa.

Akitangaza filamu zilizoingia katika kinyang’anyiro hicho Mkurugenzi wa tamasha la ZIFF, Hatibu Madudu amesema kuwa;  Tamasha hilo litahusisha maonesho ya filamu, warsha, na panorama.

“Mwaka huu tumepokea mwaka filamu 430 zilizotengenezwa kati ya mwaka 2024 na 2025 yaani filamu zilizotengenezwa ndani ya mwaka mmoja pekee kutoka nchi mbalimbali duniani zikihusisha bara la Afrika na Ulaya.” Amesema.

Madudu amesema kuwa, jumla ya filamu 174 zimewasilishwa kutoka ukanda wa Afrika Mashariki ambapo Kenya iliwasilisha filamu (54), Uganda filamu (52), Tanzania (49), Somalia nane (8), Rwanda 6, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo nne (4), na Burundi filamu moja.

Aidha amesema kuna filamu zilizowasilishwa kutoka Nchi 100 zaidi zikiwemo India, Brazil, Marekani, China, Ufaransa , Italia, Uturuki, Nigeria, Argentina, Spain, Poland, United Kingdom, Germany, Canada, Indonesia, Russia Federation, Qatar, Japan, United Arab Emirates, Pakistan, Tunisia, Angola, Malawi, Portugal, Belgium, Zimbabwe, Mayote, Vietnam, Reunion, Romania, Saudi Arabia, Oman, Morocco, Lebanon, Jamaica, Botswana, Burkina Faso, Ghana, Senegal, Sudan na Ethiopia.

Awali Mkurugenzi wa Goethe-Institut Tanzania Mpangi Otte alieleza kuwa wanajivunia kudhamini Tamasha hilo kubwa lenye hadhi ya kimataifa.

 Otte amesema Tamasha la ZIFF limebeba thamani katika ni filamu, maono pamoja na sauti zinazosimulia

hadithi za Afrika kwa upekee uliobeba sanaa na jumbe kwa jamii na kusisitiza kuwa Goethe Institut wanaamini kuwa tamaduni sio anasa bali ni kuwaleta watu pamoja na kujifunza na kupitia ZIFF Tanzania, Afrika na dunia kwa ujumla watajifunza kupitia filamu hizo, mijadala pamoja na mafunzo mbalimbali yatakayotolewa. 

Baadhi ya waandaaji na waigizaji wa filamu zilizochaguliwa katika kinyang’anyiro hicho na filamu zao kuoneshwa katika Tamasha hilo wameeleza furaha yao ya kupata fursa hiyo na kusema kuwa kupitia kazi zao jamii itapata ujumbe ambao hauwekwi wazi katika kazi nyingi za sanaa ikiwemo afya ya akili.

Cecilia Lubango, mwongozaji wa filamu ya Tears in the Rain inayohusu afya ya akili kwa wanawake waliojifungua kwa mara ya kwanza amesema ni wakati kwa 

wasanii kutumia filamu kuweka wazi matatizo yaliyopo katika jamii.

“Ninafurahi filamu hii niliyoongoza inakwenda kuoneshwa katika jukwaa kubwa la ZIFF. Hii ni mara ya kwanza kwangu, ila niwaombe wasanii wenzangu tutumie filamu kuanika matatizo katika jamii.” Ameeleza Cecilia.

Katika hatua nyingine, Mwongoza filamu ya Ndoto Yangu, Sama Johanpow, inayohusu masuala ya elimu, amesema pamoja na kupata fursa  filamu yake kuonesha katika Tamasha la ZIFF imempa moyo na kujiona katika nafasi kubwa kwa miaka ya mbele.

Katika siku ya ufunguzi wa Tamasha hilo Juni 25 saa mbili usiku filamu itakayooneshwa ni Janani The Last Stand kutoka Uganda iliyoongozwa na Matt Bish.

Tamasha la ZIFF 2025 limedhaminiwa na Umoja wa Ulaya (EU), Azam Media Ltd, Air Tanzania na CANNEX, Serikali ya Zanzibar, Wizara ya Utalii Zanzibar, Infinity Group Zanzibar, Maru Maru Hotel, Emerson Hotel, Goethe Institut, The Box, Archipelago Restaurant na Nafasi Film Club.

Mkurugenzi wa Goethe-Institut Tanzania Mpangi Otte akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na tamasha hilo na kusema kuwa  wanajivunia kudhamini tamasha hilo kubwa lenye hadhi ya kimataifa. Leo jijini Dar es Salaam.
Mtendaji Mkuu wa ZIFF, Joseph Mwale akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya tamasha la ZIFF 2025 na kueleza kuwa tamasha hilo lenye kauli mbiu ya  ‘Tumaini linalochipukia’ yamekamilika. Leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa ZIFF, Hatibu Madudu, akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na Tamatha la ZIFF msimu wa 28 na kueleza kuwa kwa mwaka huu wamepokea filamu 430 zilizotengenezwa kati ya mwaka 2024 na 2025 kutoka nchi mbalimbali duniani. Leo jijini Dar es Salaam.
Kutoka kushoto; Mkurugenzi wa Goethe Institut Tanzania Mpangi Otte, Mtendaji Mkuu wa ZIFF Joseph Mwale, Mkurugenzi wa ZIFF, Hatibu Madudu na Mwakilishi wa Bodi ya Wakurugenzi, wakionesha nembo itakayotumika katika maonesho ya ZIFF mwaka huu.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...