Serikali kupitia Wakala wa barabara Tanzania(TANROADS) Mkoani Ruvuma,imeanza kufanya matengenezo makubwa ya barabara zinazoelekea kwenye maeneo ya uzalishaji ikiwemo maeneo yanayolimwa zao la kahawa ili kutoa fursa kwa wakulima kusafirisha mazao yao kwa urahisi pindi wanapohitaji kupeleka sokoni.

Barabara ambazo zimeanza kufanyiwa matengenezo zinaunganisha Wilaya ya Mbinga na Nyasa ambazo ni maarufu kwa kilimo cha zao la kahawa ambalo ni nguzo muhimu kiuchumi kwa wananchi,na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla, kufanyika kwa urahisi ili kuwahi masoko yaliyopo kwenye maeneo ya mjini.

Kaimu Meneja wa Tanroads Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Fedinand Mdoe amesema,miongoni mwa barabara zinazofanyiwa matengenezo ni barabara ya Nyoni-Mpapa-Mkenda yenye urefu wa kilometa 108.52 inayounganisha Wilaya ya Mbinga na Nyasa.

Amesema,katika barabara hiyo kazi zinazofanyika ni matengenezo ya kawaida urefu wa kilometa 80.52 na Serikali kupitia Tanroads imetenga Sh.milioni  421,260,000.

Aidha amesema,wanafanya matengenezo sehemu korofi kilometa 27 kwa gharama ya Sh.milioni  763,368,000 pamoja na kujenga kingo  ya madaraja 3  kazi itakayogharimu Sh.milioni 60.046.

Mdoe ametaja kazi nyingine zinazofanyika katika barabara hiyo ni ujenzi wa makalavati 2 kwa gharama ya Sh.milioni 288.051 kazi inayotarajiwa kukakamilika mwezi Septemba mwaka huu.

Pia amesema,wameanza matengenezo ya maeneo mabovu kwenye barabara ya Nyoni-Mpapa-Maguu yenye urefu wa kilometa 30 na barabara ya Mbinga-Mkiri.

Amesema,katika barabara hiyo kazi zinazofanyika ni kuweka lami kwenye miinuko na maeneo korofi kutokana na  umuhimu wa barabara hiyo kiuchumi kwa wananchi wa Wilaya ya Mbinga na Wilaya ya Nyasa.

“Barabara nyingine zinazofanyiwa matengenezo ni Mbambabay-Lituhi ambayo iko kwenye ukarabati mkubwa,kuna kazi ya dharura inayoendelea katika eneo ya Lwika takribani kilometa 15 kutoka Mbambabay,tutaboresha  kwa kuinua tuta na kujenga box kalavati na kumwaga changarawe”alisema Mdoe.

Kwa mujibu wa Mdoe,barabara ya Nang’ombo kwenda Chiwindi nayo  inafanyiwa matengenezo kwa kuweka kifusi,lakini changamoto kubwa ni  magari yenye uzito mkubwa hasa yanayobeba makaa ya mawe kupitia kwenye daraja la chuma.

“tunawaomba wenzenu makampuni yanayojishughulisha na uchimbaji wa makaa ya mawe,kuzingatia sheria  kwa kutozidisha uzito kwenye magari yao,wasijali biashara yao  badala yake waangalie maslahi ya watu wengine ambao ni watumiaji wa barabara  ile”alisisitiza Mdoe.

“kimsingi kazi zetu nyingi tutazikamilisha mwaka huu wa fedha,zile barabara chache za kipaumbele tutaendelea nazo hadi mwezi Septemba mwaka 2025”alisema Mdoe.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...