Na Mwandishi Wetu

NCHI za Tanzania na Zambia zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta ya masoko ya mitaji, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukuza ujumuishaji wa kiuchumi wa kikanda na kuchochea maendeleo endelevu.

Ushirikiano huo unalenga kuongeza uwekezaji, kuboresha mifumo ya udhibiti, na kuimarisha mifumo ya usuluhishi wa migogoro kupitia mabaraza ya masoko ya mitaji ya nchi hizo mbili.

Mpango huo unaendana na maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye mara kwa mara amesisitiza umuhimu wa masoko ya mitaji kama kichocheo cha ukuaji wa uchumi na njia mbadala ya kupata fedha kwa ajili ya maendeleo.

Katika taarifa iliyotolewa na Baraza la Masoko ya Mitaji (CMT), jana ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu na Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza hilo, Dk Ntemi Kilekamajenga, upo nchini Zambia kwa ziara ya mafunzo ya siku tano kuanzia Juni 16 hadi 20, 2025.

Ziara hiyo inaambatana na mazungumzo ya ngazi ya juu na taasisi mbalimbali ikiwemo Tume ya Usalama wa Mitaji na Hisa ya Zambia (SEC), Soko la Hisa la Lusaka (LuSE), Chama cha Masoko ya Mitaji Zambia (CMAZ), pamoja na baadhi ya wajumbe wa mahakama.

Akizungumza kuhusu ziara hiyo, Msajili wa Baraza la Masoko ya Mitaji, Martin Kilikoli lisema inalenga kubadilishana uzoefu, kuimarisha ushirikiano wa kikanda, na kuchambua maeneo ya kufanya maboresho ya kisheria na kiudhibiti.

“Maeneo muhimu yanayolengwa ni pamoja na kuboresha mifumo ya utatuzi wa migogoro, kuimarisha uwazi wa masoko, na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa sekta mambo ambayo ni msingi wa kuvutia wawekezaji wa ndani na nje,” alisema.

Aliongeza hatua hiyo inaendana na mkakati wa Serikali wa kuimarisha taasisi za kisheria na kuifanya mifumo ya kifedha kuwa jumuishi na rafiki kwa wawekezaji.

“Masoko ya mitaji madhubuti ni nyenzo muhimu za kuendeleza uchumi jumuishi na endelevu,” alisema Kilikoli.

Aliongeza kuwa ushiriki wa viongozi waandamizi katika ziara hiyo unaonesha dhamira ya dhati ya Serikali katika kukuza ushirikiano wa kikanda na kuimarisha uwezo wa kitaasisi katika sekta ya masoko ya mitaji.

Kupitia ushirikiano huo, Tanzania na Zambia zinatazamiwa kushirikiana katika mageuzi ya kimfumo, kuboresha ulinzi wa wawekezaji na kuhakikisha masoko yanakuwa imara, wazi na shirikishi.

“Dira yetu ya pamoja ni kuwa na masoko ya mitaji yaliyo wazi, yanayojumuisha kila kundi na yaliyo chini ya usimamizi madhubuti, ili kujenga imani kwa wawekezaji na kuchochea maendeleo ya muda mrefu,” alisisitiza.

Hatua hii ni sehemu ya juhudi za Tanzania kujenga uchumi unaojumuisha watu wote na unaotegemea mifumo imara ya kifedha kama msingi wa maendeleo ya kitaifa na kikanda.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...