Dar es Salaam, Tanzania – Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania (TPBA) kimeingia makubaliano rasmi ya ushirikiano na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), yakilenga kuongeza mshikamano, weledi na ufanisi katika utekelezaji wa masuala ya sheria nchini.

Makubaliano hayo yamesainiwa leo jijini Dar es Salaam na viongozi wa vyama hivyo, mbele ya Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi, ambaye amesisitiza umuhimu wa utekelezaji wa makubaliano hayo kwa vitendo.

"Ni muhimu kuona haya makubaliano yakitekelezwa kwa manufaa ya pande zote mbili. Hili litasaidia kuimarisha mifumo ya sheria na utoaji wa haki nchini," amesema Dkt. Possi.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa vyama husika, ushirikiano huo utahusisha maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na mafunzo ya pamoja, kubadilishana uzoefu, na kufanya kazi kwa pamoja katika masuala ya kitaaluma na ya kitaifa.

Rais wa TLS, Wakili Boniface Mwambukusi, amesema makubaliano hayo ni fursa adhimu kwa wanasheria wa pande zote kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na kushirikiana katika kuijenga Tanzania yenye haki, amani na utulivu.

"Tunaamini kuwa kupitia ushirikiano huu, tutaimarisha taaluma ya sheria na kujenga taifa lenye mfumo wa haki unaoeleweka kwa wote," amesema Mwambukusi.

Naye Makamu wa Rais wa TPBA, Wakili Debora Mcharo, amesema makubaliano hayo yamekuja katika wakati muafaka ambapo kuna haja ya kuwa na jukwaa la pamoja la kushughulikia changamoto za kisheria nchini.

"Tunatambua nafasi ya kila upande katika kukuza misingi ya haki na utawala wa sheria. Ushirikiano huu utatupeleka mbali zaidi," amesema Mcharo.

Makubaliano haya yanatarajiwa kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya sheria kwa kuimarisha uhusiano kati ya mawakili wa serikali na wale wa upande binafsi, hali itakayosaidia kuongeza ufanisi, uwajibikaji na matumizi bora ya taaluma ya sheria nchini.

Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi (aliyesimama katikati) akishuhudia utiaji saini wa Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano baina ya Chama cha Mawakili wa Serikali, PBA na Chama cha Mawakili wa Tanganyika, TLS uliofanyika jijini Dar es Salaam leo. Kushoto anayesaini ni Katibu wa PBA, Wakili Rashid na kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa TLS, Bi. Mariam Othuman. Wanaoshuhudia nyuma ni Rais wa TLS, Wakili B. Mwabukusi na Makamu wa Rais wa PBA, Wakili Debora Mcharo.

Katibu wa Chama cha Mawakili wa Serikali (PBA), Wakili Rashid Mohamed wakibadilishana Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano na Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS), Bi. Mariam Othuman baada ya kusaini hati hiyo wakati wa hafla iliyofanyika Jijini Dar es Salaam leo. Wanaoshuhudia nyuma ni Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi (aliyesimama katikati), Rais wa TLS, Wakili Boniphace Mwabukusi na Makamu wa Rais wa PBA, Wakili Debora Mcharo (wa kwanza kulia)

Katibu wa Chama cha Mawakili wa Serikali (PBA), Wakili Rashid Mohamed na Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS), Bi. Mariam Othuman wakionesha Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano baada ya kusaini hati hiyo wakati wa hafla iliyofanyika Jijini Dar es Salaam leo. Wanaoshuhudia nyuma ni Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi (aliyesimama katikati), Rais wa TLS, Wakili Boniphace Mwabukusi na Makamu wa Rais wa PBA, Wakili Debora Mcharo (wa kwanza kulia)





Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa hafla ya utiaji saini hati ya Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) kati ya Chama cha Mawakili wa Serikali (PBA) na Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS) wakati wa mkutano na waandishi hao uliofanyika Jijini Dar es Salaam leo.



Rais wa Chama Cha Mawakili wa Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa hafla ya utiaji saini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano kati ya Chama cha Mawakili wa Serikali (PBA) na Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS) wakati wa mkutano na waandishi hao uliofanyika Jijini Dar es Salaam leo.

Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi (aliyesimama katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa Chama cha Mawakili Wa serikali (PBA), Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS) na viongozi waandamizi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali baada ya kushuhudia utiaji saini Hati ya Makubaliano ya Ushiriano baina ya vyama hivyo viwili wakati ya hafla hiyo iliyofanyika Jijini Dar es Salaam leo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...