Songea – Ruvuma.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesema kuwa takribani asilimia 70 ya bajeti kuu iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya shilingi Tirioni 56 inatokana na kodi zinazokusanywa na taasisi hiyo, hivyo kuonesha umuhimu mkubwa wa kodi katika uendeshaji wa shughuli za maendeleo nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano kutoka TRA Richard Kayombo Juni 26, katika kikao maalum na wadau wa kodi kilichofanyika Ofisi za TRA mkoani Ruvuma, chenye lengo la kuhamasisha ulipaji sahihi wa kodi na kusikiliza changamoto za walipakodi.

Kayombo amesema kuwa lengo la kikao hicho ni kutoa mrejesho kuhusu hali ya ukusanyaji wa mapato, pamoja na kuwashukuru walipakodi kwa mchango wao katika mwaka wa fedha unaoelekea tamati, Amebainisha kuwa Mkoa wa Ruvuma umeonesha mwitikio chanya katika ulipaji wa kodi, na mwenendo wa makusanyo unaridhisha.

Akisisitiza dhamira ya TRA kuwa karibu na walipakodi, Kayombo amesema kuwa Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, ameweka mkazo katika kuhakikisha walipakodi wanasikilizwa, na matatizo yao yanapatiwa majibu kwa wakati. Ameongeza kuwa, kwa mtu yeyote mwenye changamoto ya ulipaji kodi, TRA imefungua milango ya majadiliano kwa njia ya makubaliano ya kulipa kwa awamu.

Katika maelezo yake, Kayombo amewahimiza wadau wa kodi kushiriki kikamilifu katika maboresho ya sheria za kodi, kwa kuwasilisha maoni yao kila mwaka ifikapo Disemba, amesisitiza kuwa sheria za kodi hubadilika kila mwaka, hivyo ushiriki wa walipakodi katika mapendekezo ni njia mojawapo ya kuboresha mazingira ya biashara na ulipaji kodi.

Akijibu swali la mmoja wa wadau Salvatory Mangasira, Mwenyekiti wa Madereva Bajaji wa Songea kuhusu kupanda kwa bei za bajaji zinapoingia nchini, Kayombo ameeleza kuwa ushuru wa forodha ni suala la kikanda, linaloratibiwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki, ameongeza kuwa bei za bidhaa huchangiwa na mambo mengi, ikiwa ni pamoja na gharama za usafirishaji, ushuru mbalimbali, na faida ya wauzaji.

Kwa upande wake Meneja wa TRA Mkoa wa Ruvuma Nicodemus Mwakilembe, amesema kuwa kwa mwaka wa fedha unaoelekea tamati, TRA mkoani humo imekusanya zaidi ya shilingi bilioni 44, na matarajio yao ni kufikia bilioni 46 baada ya mwaka wa fedha 2024/2025 kukamika, amesema mafanikio hayo yametokana na utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kukusanya kodi kwa njia ya diplomasia bila kutumia nguvu wala msukumo usio wa lazima.

Michael West mmoja wa walipakodi alitoa pongezi kwa TRA kwa kuvuka malengo ya makusanyo, na kusisitiza kuwa hatua hiyo inadhihirisha matumizi mazuri ya kodi, akitolea mfano wa miradi ya maendeleo kama vile kusainiwa mkataba wa ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami ya Likuyufusi–Mkenda, Alisema kuwa miradi hiyo ni ushahidi wa namna kodi za wananchi zinavyosaidia maendeleo ya taifa.

TRA imeendelea kuimarisha ushirikiano wake na walipakodi kwa kusikiliza maoni, kusuluhisha changamoto, na kuhakikisha makusanyo ya kodi yanafanyika kwa njia ya haki na kistaarabu, Kwa msingi huo, mafanikio ya mapato si tu ishara ya ufanisi wa TRA, bali pia ushahidi wa uelewa na ushiriki wa wananchi katika kuchangia maendeleo ya taifa. Kwa pamoja, Serikali na walipakodi wanaweza kufanikisha malengo ya kitaifa ya uchumi imara, miundombinu bora na ustawi wa jamii kwa ujumla.










Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...