Na Jane Edward, Arusha

Wafamasia zaidi ya elfu moja kutoka mikoa mbalimbali nchini wamekutana jijini Arusha katika ukumbi wa AICC kwa ajili ya mkutano mkuu wa 55 wa Chama cha Wafamasia Tanzania, unaolenga kuimarisha maadili na weledi katika taaluma ya famasia.

Akizungumza wakati wa mkutano huo, Mwenyekiti wa chama hicho, Benson Katundu, amesema mkusanyiko huo umebeba dhamira ya kuimarisha msingi wa uadilifu, uwajibikaji na huduma bora kwa wananchi, hususan katika usimamizi wa dawa na vifaa tiba.

"Tunalenga kujenga taaluma yenye uwazi, uaminifu na weledi wa hali ya juu ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma salama, sahihi na zenye viwango stahiki," amesema Katundu.

Mkutano huo pia unatoa nafasi kwa wadau wa sekta ya afya kubadilishana uzoefu, kujadili changamoto na kuweka mikakati ya pamoja katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta ya famasia nchini.

Kaulimbiu ya mkutano wa mwaka huu ni "Maadili, Weledi na Uwajibikaji: Nguzo ya Huduma Bora za Famasia kwa Maendeleo ya Taifa", ikilenga kuhimiza wafamasia kuwa mstari wa mbele katika kutoa huduma zenye kuzingatia utu, usalama wa mgonjwa na ufanisi wa kitaaluma.

Wadau mbalimbali wa sekta ya afya walioudhuria mkutano huo, wakiwemo wawakilishi kutoka JD Pharmas, MSD (Medical Stores Department) na CSSC (Christian Social Services Commission), wamesema wamefurahia nafasi ya kukutana na wadau tofauti kutoka kila kona ya nchi. Wameeleza kuwa mkutano huu umefungua fursa ya ushirikiano na mawasiliano kati ya sekta binafsi, ya umma na mashirika ya kijamii katika kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya.

Mkutano huo wa siku kadhaa unatarajiwa kuibua maazimio muhimu yatakayosaidia kuimarisha mfumo wa utoaji huduma za afya nchini kupitia taaluma ya famasia.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...