Na Farida Mangube, Kilosa, Morogoro
Wakazi zaidi ya 2,000 wa Kijiji cha Mahemu, kilichopo Kata ya Mtumbatu, Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, wanatarajia kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya baada ya kuanza rasmi ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho.
Kwa zaidi ya miaka 15 tangu kuanzishwa kwake, kijiji hicho hakijawahi kuwa na zahanati, jambo ambalo limekuwa likihatarisha maisha ya wananchi, hususan wanawake wajawazito, watoto na wazee huku wakazi walilazimika kusafiri kwenda vijiji jirani kutafuta huduma za msingi, ikiwa ni pamoja na huduma za mama na mtoto.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wakati wa zoezi la kuchimba msingi wa zahanati hiyo, Diwani wa Kata ya Mtumbatu, Mheshimiwa Amani Sewando alisema juhudi za kuanza ujenzi huo ni sehemu ya dhamira ya kujiletea maendeleo kwa kushirikiana na serikali.
“Kwa muda mrefu tumekuwa tukikumbwa na changamoto ya wanawake kujifungulia njiani kwa kukosa huduma za karibu. Zahanati hii itapunguza kwa kiasi kikubwa adha hiyo na kusaidia kuokoa maisha,” alisema Mh. Sewando.
Katika kuunga mkono juhudi za wananchi, Mheshimiwa Sewando alichangia mifuko 100 ya saruji ili kufanikisha hatua za awali za ujenzi wa zahanati hiyo.
Ujenzi huu unakwenda sambamba na Sera ya Wizara ya Afya inayolenga kusogeza huduma za afya karibu na wananchi, kwa mujibu wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025. Sera hiyo inalenga kuhakikisha kila kijiji au mtaa unakuwa na kituo cha afya cha msingi ili kuongeza upatikanaji wa huduma kwa wananchi wote bila kujali mazingira yao ya kijiografia.
Aidha, juhudi hizi ni mchango muhimu katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hasa Lengo la 3 linalohimiza afya bora na ustawi kwa wote. Kupitia lengo hilo, nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zimepania kupunguza vifo vya uzazi, kuongeza huduma jumuishi za afya na kuhakikisha kila mtu anapata huduma za msingi ifikapo mwaka 2030.
Wananchi wa Mahemu wamekuwa mstari wa mbele kuchangia fedha, vifaa vya ujenzi na nguvu kazi ili kufanikisha mradi huo. Hata hivyo, wameiomba serikali na wadau wa maendeleo kuwasaidia kukamilisha ujenzi huo haraka iwezekanavyo.
“Tunaiomba serikali ituunge mkono kwa kutupatia vifaa vya ujenzi vilivyosalia pamoja na watumishi wa afya mara tu zahanati itakapokamilika. Tuna moyo wa kujitolea, lakini uwezo wetu ni mdogo,” alisema Mzee Ramadhani Mshana, mkazi wa kijiji hicho.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...