*Asema wanaosema hakuna kilichofanyika hawana tofauti na Kasuku
Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Michuzi Blog
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira amesema tangu kupata uhuru Tanzania imepata maendeleo makubwa na wanaosema hakuna kilichofanyika ni vema wakakaa kimya, wasiwe na tabia ya kasuku kukariri wasiyoyajua.
Wasira ameyasema hayo leo Juni 17, 2025 alipokuwa akizingumza katika mkutano wa hadhara Katoro, mkoani Geita akiwa katika ziara ya kukagua uhai wa Chama na kuzungumza na wananchi.
Akieleza kuhusu maendeleo yaliyofanyika nchini tangu kupatikana kwa uhuru alisema ni makubwa na wenye umri mkubwa wanajua vizuri nchi ilivyokuwa na wamekuwa wakishuhudia hatua mbalimbali zinazofanywa na serikali inayoundwa na CCM.
“Labda ninyi vijana hamwelewi lakini niwaambie wakoloni wa Kijerumani na wakoloni wa Kiingereza wamekaa Tanganyika miaka 75, Wajerumani wamekaa miaka 35, wamejenga reli kwa viboko bila malipo.
“Waingereza wamekaa miaka 40 walitumwa na Umoja wa Mataifa (UN) watuendeleze tujitawalie, lakini miaka 40 ya Waingereza wametuacha na wahandisi wawili katika nchi isiyo na barabara.
“Wametuachia nchi hakuna daktari hata mmoja walikuwepo madaktari kutoka India na Pakistani nao walikuwa Dar es Salaam. Wakati tunapata uhuru akina mama walikuwa hawajifungui ila wanazaa maana hakukua na kliniki.
“Hivyo walikuwa wanazaa kama ng’ombe anavyozaa ndama. Ng’ombe umeona wapi ana kliniki (ya uzazi)? Hiyo ndio hali waliyotuacha nayo (wakoloni) wametuacha hatuna barabara.
“Leo anakuja mtu hajafikisha umri wa miaka 30 au miaka 40 anawaambia hakuna maendeleo. Wewe uliwahi kutembea kwa miguu, kuna maendeleo, hao wanaosema hakuna maendeleo ambayo yamefanyika akija muulizeni hivi kwako maendeleo ni kitu gani?”amesema Wasira.
Amesema inawezakana wanaosema hakuna kilichofanyika anazungumza kama kasuku, maana kasuku huwa anakariri tu haelewi hata maana ya maneno anayosema na hao ndio wanasiasa wapya, sisi wakati tumejitawala tulikuwa na msomi mmoja tu mwenye ‘Master’ (shahada ya uzamili) Julius Nyerere ndio alikuwa ameandaliwa na Wakoloni kwa miaka 75.
“Leo wala sio Tanganyika nilikuwa namuuliza Mkurugenzi wa Bukombe asubuhi anasema ana wahandisi 12, nikasema wewe ni tajiri kuliko Tanganyika ya mwaka 1970 maana kulikuwa na wahandisi wawili wewe unao 12. Namuuliza madaktari anasema wengi tu sisi hatukuwa na daktari.
“Hiyo ndio nchi tuliyorithi, leo unaweza kwenda mkoa wowote wa Tanzania kwa lami. Zamani wakati tunakabidhiwa nchi lami ilikuwa inatoka Dar es Salaam mpaka Morogoro kwa sababu kulikuwa na wazungu wanalima mkonge, ilikuwa inatoka Tanga mpaka Korogwe kwa sababu kulikuwa na wazungu wanalima mkonge.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...