Dar es Salaam. Tarehe 23 Juni 2025: Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano ambaye pia ni Mbunge wa Ilala, Mheshimiwa Mussa Zungu amesema kutokana na vifaa vya kisasa vitakavyofungwa katika Shule ya Mfano ya Benki ya CRDB basi itakapokamilika na kuanza kupokea wanafunzi itazalisha wahitimu wenye ujuzi unaohitajika sokoni.

Shule hiyo inayojengwa katika Manispaa ya Ilala, inatarajiwa kuwa na madarasa 16 ya kisasa, maabara nne  zitakazochochea ubunifu, maktaba moja kwa ajili ya kupanua maarifa, chumba kimoja cha TEHAMA, ofisi 11 za walimu na wafanyakazi pamoja na maliwato 53 zikiwamo 48 kwa ajili ya wanafunzi na 5 za wafanyakazi bila kusahau viwanja vya michezo.

“Namshukuru mkurugenzi mtendaji wa Benki ya CRDB kwa kukubali kuunga mkono juhudi za serikali za kuboresha elimu nchini na kuichagua Wilaya ya Ilala kuijenga shule hii ya mfano. Tunaamini madarasa 16 na maabara zake ikiwemo ya TEHAMA yatasaidia kwa kiasi kikubwa kuwaandaa vijana wetu kuingia kwenye soko la ajira wakiwa na ujuzi unaohitajika. Nawashukuru sana Benki ya CRDB,” amesema Mheshimiwa Zungu.
Naibu Spika Zungu ametoa pongezi hizo mwishoni mwa wiki alipotembelea eneo inapojengwa shule hiyo akiambatana na viongozi wa Jiji la Dar es Salaam.

Akimweleza Mheshimiwa Zungu kuhusu mradi huo utakaotekelezwa kwa kati ya miezi 10 mpaka miezi 12, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema maandalizi yote muhimu yamekamilika na mkandarasi, kampuni ya Juin Company Limited, ameidhinsihwa na pande zote mbili kuanza utekelezaji wa majukumu yaliyo mbele yake.

“Benki ya CRDB inavyo viwango vyake ambavyo tungependa shule hii ya mfano iwe navyo pia. Kuanzia kwenye mwonekano mpaka ubora wa vifaa vya ujenzi. Ni matarajio yangu kwamba mkandarasi utafanya kazi kadri ya makubaliano ili mradi huu ukamilike kwa wakati kama tulivyokubaliana. Tutapenda kuona value for money (thamani ya fedha) sio kusikia maneno ya aina yoyote yatakayomaanisha kuchelewesha kazi hii,” amesema Nsekela.

Jiji la Dar es Salaam lina jumla ya shule za msingi 1,016 zikiwamo 419 zinazomilikiwa na serikali na 597 za watu au taasisi binafsi pamoja na sekondari 379 zinazojumisha 197 za serikali. Ujenzi wa shule hiyo ya mfano, utaongeza idadi ya sekondari zilizopo jijini humo na kufika 380.
“Ingawa shule hii itamilikiwa na serikali lakini ujenzi wake unasimamiwa na Benki ya CRDB na utabeba jina la benki yetu hivyo ujenzi wake lazima uwe na viwango vikubwa. Ikiwezekana, shule zitakazojengwa hapo baadaye zije kujifunza hapa,” amesema Nsekela.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam,  Elihuruma Mabelya amesema halmashauri yake in shule 118 na hii inayojengwa na Benki ya CRDB itakuwa ya 119. Shule hizi zilizopo, amesema zinawahudumia zaidi ya wanafunzi 100,000 hivyo zinahitajika shule nyingine nyingi zaidi ili kukidhi mahitaji yaliyopo na yanayozidi kuongezeka kila siku.

“Nawashukuru Benki ya CRDB katika utekelezaji wenu wa sera ya uwekezaji kwa jamii uliowezesha kutujengea shule hii ya mfano. Pia, nimpongeze Naibu Spika kwa juhudi zake za kuhakikisha tunapata shule hii itakayojengwa kwa hela nyingi,” ameshukuru Mabelya.

Katika jitihada za kuimarisha miundombinu ya elimu jijini Dar es Salaam, serikali imejenga shule nane za ghorofa na katika mwaka ujao wa fedha, Mstahiki Meya wa Jiji, Omary Kumbilamoto amesema “zitajengwa nyingine 10.”

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...