NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV

Tanzania imeandaa Mkutano wa 27 wa Kamati ya Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuhusu Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama (Ministerial Committee of the Organ – MCO), unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo umefunguliwa leo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel W. Shelukindo, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu ya MCO.

Akiwahutubia wajumbe wa mkutano huo, Dkt. Shelukindo alisisitiza umuhimu wa mshikamano wa kikanda katika kuimarisha amani, usalama na utulivu ndani ya ukanda wa SADC.

“Ni fursa muhimu kutathmini maendeleo ya utekelezaji wa maamuzi mbalimbali ya Mikutano ya Wakuu wa Nchi, Baraza la Mawaziri, pamoja na maazimio ya mkutano uliopita wa 26 uliofanyika Lusaka, Zambia, Julai mwaka jana,” alisema Dkt. Shelukindo.

Aidha, mkutano huu unatarajiwa kujadili taarifa kutoka kamati mbalimbali ikiwemo Kamati ya Kisiasa na Kidiplomasia, Kamati ya Ulinzi na Usalama, Kamati Ndogo ya Usalama wa Ndani, Kamati ya Mapambano dhidi ya Rushwa, Kamati ya Magereza, SARPCO (Polisi wa Kikanda), pamoja na Kamati ya Usalama wa Taifa.

Miongoni mwa masuala yatakayojadiliwa ni pamoja na hali ya usalama Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambako kikosi cha SADC kipo katika operesheni ya kulinda amani kupitia ujumbe wa SAMIDRC.

Dkt. Shelukindo alitumia nafasi hiyo pia kutoa pole kwa vifo vya viongozi wa zamani wa SADC akiwemo Rais wa zamani wa Zambia, Mheshimiwa Edgar Chagwa Lungu, na Makamu wa Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Mheshimiwa David Mabuza. Mkutano ulisimama kwa dakika moja kuwaombea marehemu hao.

“Tunawakumbuka kwa mchango wao mkubwa katika kujenga mshikamano wa kikanda. Walikuwa viongozi waliotanguliza maslahi ya umoja na maendeleo ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara,” alisema.

Aliongeza kuwa SADC itaendelea kuwaenzi wanajeshi waliopoteza maisha wakiwa kwenye majukumu ya kulinda amani nchini DRC.

Mkutano huo wa siku tano unalenga kuweka mikakati imara ya kushughulikia changamoto za kisiasa na kiusalama, sambamba na kuimarisha uhusiano wa nchi wanachama wa SADC katika nyanja za kisekta.








Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...