Na Diana Byera – Bukoba


Shirika lisilo la kiserikali linaloshughulika na masuala mbalimbali ya kilimo cha mazao, Cafe Africa, linatarajia kujenga uwezo na kutoa huduma za ugani kwa wakulima wa kahawa zaidi ya 35,000 ili kuendelea kufikia malengo makubwa ya kuzalisha kahawa yenye ubora nchini na kufikia malengo yaliyokubaliwa na nchi 25 zinazozalisha kahawa katika Bara la Afrika.

Katika hafla ya kufanya uzinduzi wa mradi wa uzalishaji endelevu wa kahawa aina ya Robusta mkoani Kagera kwa awamu ya pili, Meneja wa shirika hilo, Samora Mnyaonga, alisema kuwa mradi huo kwa awamu ya kwanza ulifanyika mkoa wa Kagera kuanzia mwaka 2020 hadi 2024 kwa lengo la kufufua mashamba mapya na kujenga uelewa kwa wakulima juu ya ubora wa kilimo cha kahawa.

Alisema kuwa mradi wa kwanza ulibadilisha fikra nyingi sana za wakulima, hasa waliokuwa na mibuni ya miaka 100 hadi 200 shambani, baada ya kubadili mtazamo wa kilimo cha kisasa na kubadili mibuni yao kuwa ya kisasa na kupata mavuno mengi jambo ambalo lilivutia kaya nyingi mkoani Kagera na kuongeza kiwango cha mavuno kwa mwaka.

Alisema baada ya kufanya kazi kwa miaka mitano na kuona mabadiliko makubwa, wafadhili wa shirika hilo ambao ni wabobezi wa masuala ya kahawa ulimwenguni, JDE Peet’s na Jacobs, walivutiwa na sera za serikali mkoani Kagera juu ya kupunguza umasikini kupitia zao la kahawa na kuamua tena kufadhili mradi wa awamu ya pili kuanzia mwaka 2025 hadi 2029.

Alisema utekelezaji wa mradi huu awamu ya pili unalenga kuongeza huduma za ugani, mafunzo na uelimishaji juu ya uzalishaji wa kahawa, uongezaji wa thamani katika zao hilo pamoja na ushirikishwaji kuanzia ngazi ya kaya, wadau hadi ngazi ya mkoa ili kupata zao bora la kahawa ambayo inahitajika sokoni.

"Katika mradi huu tutaajiri maafisa ugani wanaotoa huduma za ugani na ushauri 500, wakulima viongozi 300, mashamba darasa 300, wataalamu wa kutoa ushauri watakaoungana na watafiti kutoa huduma kwa wakulima watafikia 200," alisema Mnyaonga.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa, alisema kuwa amevutiwa na mipango ya shirika hilo kwani limeunga mkono juhudi mahususi za mkoa wa Kagera za kuhakikisha kila mkazi wa Kagera ananufaika na kilimo cha kahawa bila kujali umri.

Alisema mkoa umefikia jitihada za makusudi za kuongeza uzalishaji hadi kufikia tani 200,000 ifikapo mwaka 2030, ambapo kwa kuanza tu, mkoa utawapitia vijana 10,000 maeneo ya kilimo kama sehemu ya kuwaongezea kipato.

"Nalipongeza shirika hili kwa kuja na mpango mzuri wa kuunga jitihada za mkoa. Baada ya kuona kilimo cha kahawa kinapesa, mkoa umekuja na mkakati wa kutoa hekari moja moja kwa vijana 10,000 bila kuwahamisha makazi kwa kuwalimia, kuwapa miundombinu, hatimiliki na kila kitu hekari moja ili iwe urithi wa kudumu, hata akiwa na familia, lile shamba litakuwa lake na familia yake," alisema Mwassa.

Meneja wa Bodi ya Kahawa mkoani Kagera, Edmond Zan, kwa niaba ya Meneja wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), alisema kuwa serikali nchini ilipata kiasi cha shilingi bilioni 537 zilizotokana na mauzo ya kahawa.

Alisema mikakati ya wadau inalenga kuwainua wakulima na kuongeza uzalishaji, huku akisisitiza kuwa ni vyema wakulima wa Kagera wanatumia fursa hiyo vizuri, hasa kuzingatia ubora wa kahawa ili kunufaika na soko la dunia.












Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...