NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

Mkuu wa Usalama Barabarani Chang’ombe, Reverent Nkyami amesema ukosefu wa elimu rasmi na mafunzo ya usalama barabarani umechangia waendeshaji wengi wa pikipiki kuendesha vyombo hivyo kiholela bila kuzingatia sheria, hali inayochochea ongezeko la ajali na vifo barabarani.

Ameyasema hayo leo Julai 19, 2025 JIjini Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi wa kilainishi kipya cha Caltex Ezy 4T Plus.

“Kumekuwa na tabia ya kujifunza siku mbili tu mitaani, kesho mtu anaingia barabarani bila uelewa wa sheria. Mbaya zaidi anapakia abiria zaidi ya uwezo (‘mishikaki’), hana stadi ya kuendesha kwa usalama na mwisho wa siku anagongwa au anasababisha vifo,” alisema Nkyami.

Aliongeza kuwa Jeshi la Polisi limeendelea na juhudi za kutoa elimu kwa waendesha vyombo vya moto pamoja na kufanya oparesheni mbalimbali, zenye lengo la kuongeza uelewa kwa madereva na kupunguza ajali barabarani.

“Asilimia kubwa ya ajali zinahusisha pikipiki, iwe ni dhidi ya waenda kwa miguu, magari au hata pikipiki kwa pikipiki. Hivyo tumejikita katika kutoa elimu zaidi kwa bodaboda ili kukomesha hali hiyo,” alibainisha.

Aidha, aliwataka waendesha pikipiki kushiriki kikamilifu kwenye mafunzo yanayoendeshwa na Jeshi hilo ili kuongeza maarifa, weledi na kuwa salama wawapo barabarani.

Kwa upande mwingine, uzinduzi wa kilainishi kipya cha Caltex Ezy 4T Plus uliambatana na uzinduzi wa kampeni ya usalama barabarani kwa waendesha bodaboda na bajaji. Kilainishi hicho kimetengenezwa kwa teknolojia ya kisasa na kimekusudiwa kupunguza gharama za matengenezo ya vyombo vya moto.

Mkuu wa Kitengo cha Vilainishi kutoka Kampuni ya Karimjee Value Chain Limited, Anam Mwemutsi, alisema bidhaa hiyo mpya imekuja kupambana na tatizo sugu la uchakachuaji wa vilainishi linalosababisha uharibifu wa injini za pikipiki.

“Tumeleta kilainishi chenye uwezo wa kusafiri hadi kilomita 5,000 bila kubadilishwa, tofauti na sasa ambapo wengi hubadilisha kila baada ya wiki moja. Hii itapunguza gharama na kuongeza ufanisi wa vyombo vya usafiri,” alisema Mwemutsi.

Naye Msemaji Msaidizi wa Shirikisho la Waendesha Bodaboda na Bajaji Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Msisiri, aliipongeza kampuni hiyo kwa kubuni suluhisho litakalosaidia kuimarisha usalama wa vyombo vya usafiri na kupunguza ajali zitokanazo na ubovu wa pikipiki.

“Tatizo la vilainishi vilivyochakachuliwa limekuwa likitutesa kwa muda mrefu. Kupatikana kwa bidhaa hii bora ni hatua kubwa kwa usalama wetu,” alisema Msisiri kwa furaha.










Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...