Iramba: Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Mheshimiwa Suleiman Mwenda ameishukuru Benki ya CRDB kwa kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya Mukulu akisema kitasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha huduma za afya kwa wananchi wa Kata ya Mukulu na maeneo jirani.

Kutokana na uhitaji kuongezeka kila siku, Mheshimiwa Mwenda amesema serikali inafanya jitihada kubwa kuboresha huduma za afya lakini inawaikaribisha sekta  binafsi kuongeza nguvu ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma katika maeneo jirani.

“Huduma za afya ni msingi wa maendeleo ya mtu binafsi, kaya mpaka taifa. Ukiwa na afya njema basi unao mtaji muhimu wa kufanikisha malengo yako na pale afya inapoyumba kidogo ni muhimu kulishughulikia tatizo husika haraka iwezekanavyo ili lisikucheleweshe kufanya mambo mengine.
Kituo hiki cha Afya Mukulu kipo kwa ajili hiyo, niwashukuru sana Benki ya CRDB kwa kutusaidia kukijenga, hakika ninyi ni benki ya mfano nchini,” amesema Mheshimiwa Mwenda.

Mheshimiwa Mwenda amesema hayo kwenye hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika katika Kijiji cha Mukulu akimwakilisha Mbunge wa Iramba ambaye ni Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba aliyeomb aujenzi wa kituo hicho cha afya kwa niaba ya wananchi.

Akielezea kutokuwapo kwa waziri aliyetarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye hafla hiyo, amesema amebanwa na majukumu mengine lakini naye anaungana na wana Iramba kwa ujumla kuishukuru Benki ya CRDB kwa kuwajali wananchi anawawakilisha bungeni.
Akikabidhi kituo hicho, Makamu Mwenyekiti wa Bodiya wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Dkt. Donald Mmari amesema ni utaratibu wa benki kutenga asilimia moja ya faida yake baada ya kodi kila mwaka ili kusaidia kutekeleza miradi inayowalenga wananchi.

“Mradi huu wa Kituo cha Afya Mukulu ni ushuhuda wa utekelezaji wa sera hiyo. Ujenzi wa kituo hiki unalenga kuboresha huduma za afya kwa wananchi na wakazi wa hapa. Ujenzi wake umefanyika kwa weledi na ushirikiano wa karibu baina yetu na halmashauri tukizingatia mahitaji halisi ya wananchi wa hapa Mukulu na Wilaya nzima ya Iramba,” amesema Dkt. Mmari.
Kituo hicho kilichogharimu zaidii ya shilingi milioni 180 kinatarajiwa kuwahudumia wakazi wa Mukulu pamoja na wananchi wa kata jirani kama vile Ulemo, Kyengege, Ndago na Mtoa hivyo kupunguza foleni ya wagonjwa wanaotibiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Old Kiomboi.

“Tunaamini kukamilika kwa ujenzi wa kituo hiki cha afya hapa Mukulu kutapunguza umbali ambao wananchi walikuwa wanatembea kufuata huduma za afya pamoja na gharama walizokuwa wanalazimika kuzilipia kufuata matibabu katika Hospitali ya Old Kiomboi hivyo kuongeza fursa ya watu kushiriki shughuli za uzalishaji ili kujiletea maendeleo binafsi nakuchangia uchumi wa taifa letu,” amesema Dkt. Mmari.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...