Farida Mangube, Morogoro
Wananchi kutoka mikoa ya Tanga, Pwani, Dar es Salaam na Morogoro wametakiwa kujitokeza kwa wingi kushiriki Maonesho ya kilima,ufugaji na uvuvi (Nane Nane) Kanda ya Mashariki, yatakayofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, mjini Morogoro kuanzia tarehe 1 hadi 8 Agosti 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya maonesho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Malima, amesema miongoni mwa vivutio vikubwa vya mwaka huu ni kuanzishwa kwa Jukwaa la Business to Business, litakalotoa mafunzo ya bure kwa wananchi kupitia mada mbalimbali zinazohusu kilimo, ufugaji na uvuvi.
“Mwaka huu tumeongeza msukumo katika elimu kwa vitendo. Kupitia jukwaa hili, wananchi wataweza kujifunza kila siku kutoka kwa wataalamu waliobobea kutoka taasisi za serikali na sekta binafsi,” amesema Mhe. Malima.
Kwa mujibu wa ratiba ya kamati ya maandalizi ya maonesho hayo ufunguzi rasmi utafanyika tarehe 2 Agosti 2025 na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu mstafu Mhe, Mizengo Pinda.
Mhe. Malima amesema licha ya changamoto zilizojitokeza katika miaka iliyopita, ikiwemo upungufu wa maji, mwaka huu hali ni tofauti. “Tumechimba kisima kwa kushirikiana na Wizara ya Maji, tumehakikisha huduma ya maji inapatikana kwa uhakika,” amesema Malima
Halmashauri zote kutoka mikoa ya Kanda ya Mashariki zinatarajiwa kushiriki katika maonesho hayo, pamoja na taasisi za utafiti, vyuo, mashirika ya maendeleo na wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi pamoja na wafanyabiashara na wajasiriamali mbalimbali watashiriki kuonesha bidhaa na huduma zao.
Aidha Malima amewataka wananchi wote kufika viwanjani kwa wingi kujifunza kwa vitendo. “Maonesho haya ni fursa ya kipekee kwa kila mmoja wetu. Tunawahimiza wananchi wajitokeze kujifunza, kushiriki na kufaidika na fursa mbalimbali zinazopatikana,” amesema Mhe. Malima.
Maonesho hayo hufanyika kila mwaka kwa lengo la kutoa elimu, kuhamasisha matumizi ya teknolojia, kubadilishana maarifa na kuonesha mafanikio katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...