Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri kuongeza juhudi katika kutoa hamasa kwa wananchi ili kuzingatia kanuni za afya bora na kuchukua hatua madhubuti za kujikinga na magonjwa ya kuambukiza na yale yasiyo ya kuambukiza.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akifungua Mkutano wa Mwaka wa Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete mkoani Dodoma. Amesema ni vema elimu itakayotolewa izingatie ujenzi na matumizi ya vyoo bora, unawaji mikono kwa maji tiririka na sabuni nyakati zote muhimu ili kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza, uondoshaji salama wa majitaka katika ngazi ya kaya na maeneo ya umma pamoja na kutibu maji ya kunywa kwa njia ya kuchemsha au kwa kuzingatia maelekezo ya wataalam.

Vilevile Makamu wa Rais ametoa rai kwa Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri kuvitunza vifaa tiba ikiwemo mashine za kisasa za uchunguzi na matibabu pamoja na magari ya kubeba wagonjwa yaliyonunuliwa na Serikali ili viweze kutumika kwa muda mrefu na kutoa huduma kwa watu wengi zaidi.

Pia amewasihi kuimarisha eneo la utunzaji wa kumbukumbu za matumizi ya dawa na vifaa tiba ili kuleta ufanisi katika utunzaji wa dawa na vifaa tiba na kuepuka upotevu. Amesema kutokuwepo na kumbukumbu sahihi za matumizi ya dawa na vifaa tiba hutatiza katika usambazaji wa dawa kutoka Bohari Kuu ya Dawa, na kutoa mwanya wa wizi na matumizi yasiyo sahihi.

Halikadhalika Makamu wa Rais amewaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri kulipa kipaumbele suala la utoaji wa elimu ya matumizi sahihi ya dawa ili kuisaidia jamii kutambua na kuepuka madhara ya matumizi holela ya dawa hususani dawa za maumivu na antibiotics ambazo zikitumiwa kiholela madhara yake ni makubwa. Pia amewataka kusimamia kwa ukaribu utekelezaji wa kiapo cha maadili katika kuwahakikishia wananchi huduma bora.

Aidha ameziagiza Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha zinasimamia vema ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha yanatumika kiadilifu ili kuboresha zaidi utoaji wa huduma wakati Serikali inapoelekea kutekeleza mpango wa Bima ya Afya kwa Wote.

Amesema katika kuhakikisha utoaji wa huduma bora za afya, Serikali imeweka kipaumbele suala la rasilimali watu yenye weledi, ambapo imeajiri jumla ya watumishi wapya 25,936 wa kada mbalimbali za afya katika ngazi ya msingi. Hatua hiyo imesaidia kukabili upungufu wa watumishi na kuongeza uwiano kati ya watoa huduma na wagonjwa. Ameongeza kwamba Serikali itaendelea kutoa kipaumbele katika eneo hilo hususani kwenye kada za kimkakati, ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora na endelevu kwa wananchi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, Serikali imefanikisha ujenzi wa jumla ya vituo kutolea huduma za afya 7414 ikiwemo vituo vilivyokuwepo na vilivyojengwa Awamu ya Sita. Amesema kwa miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan jumla ya hospitali kongwe 48 zimekarabatiwa, ujenzi wa majengo ya huduma za dharura 87, majengo ya huduma za wagonjwa mahututi 30 pamoja na mifumo ya hewa tiba 21.

Ameongeza kwamba katika kipindi cha miaka minne jumla ya wakinamama zaidi ya laki tisa waliokuwa wakikabiliwa na changamoto za uzazi pingamizi waliweza kufanyiwa upasuaji salama katika vituo vya afya vilivyoboreshwa na vilivyojengwa upya.

Kwa upande wake Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema Serikali imeendelea kutoa kipaumbele katika sekta ya Afya ikiwemo kuongeza bajeti kufikia trilioni 2.6 kwa mwaka wa fedha 2025/2026. Amesema kwa miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Bajeti ya Wizara ya Afya imefikia trilioni 7.15 hivyo kufanya mageuzi makubwa ya utoaji huduma za afya nchini. Amesema Wizara inatarajia kuanzisha chaneli maalumu ya Afya (Afya Tv) ili iweze kutangaza taarifa zinazohusu afya kwa wananchi.

Amesema juhudi mbalimbali katika kuboresha sekta ya afya zimesaidia kupambana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo kumaliza ugonjwa wa Marbug ndani ya muda mfupi wa siku 54, kuimarisha diplomasia ya kimataifa katika sekta ya afya, kupungua kwa vifo vya mama na mtoto, kupungua kwa vifo vinavyotokana na dharura, kuongezeka kwa tiba utalii.

Ameongeza kwamba kwa sasa Tanzania inatarajia kuwa kuwa kituo cha umahiri wa matibabu ya upandikizaji ini, kituo cha umahiri matibabu ya mfumo wa mkojo, matibabu ya uzazi kwa wanaume, akili mnemba katika upasuaji, matibabu ya damu na upandikizaji uloto, matibabu ya figo, matumizi ya nyuklia katika matibabu ya saratani.

Awali akisoma risala, Mwenyekiti wa Waganga Wakuu wa Mikoa Dkt. Best Magoma ameipongeza serikali kwa maboresho makubwa yaliyofanyika katika sekta ya afya kuanzia ngazi ya afya ya msingi. Pia ameiomba Serikali kuhakikisha inapunguza uhaba wa nyumba za watumishi katika vituo vya kutolea huduma za afya ili kukabiliana na dharura zinazowapata wananchi hususani nyakati za usiku.

Mkutano huo wa siku tatu una kauli mbiu isemayo “Wajibu wa Waganga Wakuu wa Miko ana Halmashauri katika kuimarisha Ubora wa Huduma za Afya kuelekea Bima ya Afya kwa Wote”











Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...