Mradi wa Kuboresha na Kuimarisha Elimu ya Msingi na Awali Tanzania Bara( BOOST) unaotekelezwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, umekuwa sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020/2025.

Ilani hiyo inaelekeza Serikali , kuboresha miundombinu ya elimu ya awali na msingi kwa kujenga na kukarabati madarasa, vyoo, ofisi za walimu, nyumba za walimu, pamoja na kununua samani na vifaa vya kufundishia na kujifunzia.

Katika kutekeleza maelekezo hayo, Shule ya Msingi Ilboru iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Arusha imenufaika na Program ya BOOST inayotekelezwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikishana na Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa ufadhili wa Benki ya Dunia (WB).

Kupitia program hiyo shule ya Ilboru imejengewa vyumba vinne vya madarasa na matundu sita ya vyoo, kwa gharama ya shilingi milioni 112.6 ambapo madarasa matatu yanatumika na wanafunzi wa elimu ya awali na darasa moja linatumiwa na wanafunzi wa darasa la kwanza.

Akizungumza kuhusu mafanikio hayo, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Philomena Mbiling’i, amesema shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 1,629, ambapo wavulana ni 869 na wasichana 760, na hapo awali walikabiliwa na changamoto ya uhaba wa madarasa.

“Mradi wa BOOST umeleta hamasa kubwa kwa wanafunzi wetu. Miundombinu safi na rafiki kwa mtoto imeongeza ari ya kujifunza,” alisema Mbiling’i.

Kwa upande wake, Mwalimu wa Elimu ya Awali, Anna Marti, alisema anafundisha watoto 92, wakiwemo watoto wa mahitaji maalum kama wenye ulemavu wa ngozi na viungo.

Amesema mazingira mazuri ya kujifunzia yanawawezesha watoto kuelewa kwa urahisi kupitia mbinu za michezo, hadithi, mijadala na elimu ya afya na lishe.

“Mahudhurio yameongezeka sana, na watoto wanakuwa na shauku ya kuja shule. Uboreshaji huu umeleta matokeo chanya katika elimu ya awali,” amesema Marti.

Mradi wa BOOST ni miongoni mwa jitihada za Serikali za kutekeleza Ilani ya CCM kwa vitendo, kwa kuhakikisha watoto wote wanapata elimu bora katika mazingira salama, jumuishi na rafiki kwa mtoto.

















Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...