Na Diana Byera, Bukoba

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wamezindua zoezi la kugawa majiko na mitungi ya gesi 486 kwa watumishi wote wa magereza nane za mkoa wa Kagera, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono sera ya serikali ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa Watanzania wote ifikapo mwaka 2034.

Akizindua zoezi hilo kwa watumishi 99 wa Magereza ya Bukoba kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya REA, Lucas Charles alisema kuwa serikali imeagiza magereza zote nchini kuhamia katika mfumo wa nishati safi ya kupikia na kwamba magereza zote zimetekeleza agizo hilo. Aliongeza kuwa mpango unaoendelea kwa sasa ni kuhakikisha watumishi wote wa magereza nao wanahamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia majumbani kwao.

Alisema kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha Watanzania wote wanaoishi vijijini na mijini wanatumia nishati safi ya kupikia kwa asilimia 80 ifikapo mwaka 2034, na kudai kuwa kwa sasa mwitikio wa wananchi wanaotumia nishati safi ni mkubwa.

Meneja Usaidizi wa Kiufundi REA kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa REA, Emmanuel Yesaya, alisema kuwa serikali kupitia wakala wa Nishati Vijijini REA imetenga shilingi bilioni 35 kwa ajili ya kusambaza majiko na mitungi kwa watumishi wote wa magereza nchini, ujenzi wa miundombinu ya nishati safi ya kupikia kwa magereza zote, usambazaji wa mkaa mbadala wa kupikia katika magereza zote tani 850, pamoja na ununuzi wa mashine 61 za kuzalisha mkaa mbadala wa kupikia.

Alisema lengo la serikali ni kuhakikisha mazingira yanalindwa kwa nguvu zote, kuboresha afya za Watanzania huku wakiokoa muda wa kufuata kuni na mkaa na badala yake kutumia muda mfupi kuandaa chakula, na muda uliobaki utumike kufanya kazi nyingine za uzalishaji.

Ametoa wito kwa watumishi wote walionufaika na majiko hayo kuhakikisha wanakuwa sehemu ya hamasa kwa jamii ili kupitia kwao, kiwango na idadi ya wananchi wanaotumia nishati safi iweze kuongezeka kwa kasi.

Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Magereza ambaye anakaimu ukuu wa Magereza mkoa wa Kagera, Heron Noberth, alisema kuwa tayari magereza zote za mkoa wa Kagera zinatumia nishati safi ya kupikia tangu waliposaini mkataba na serikali na utekelezaji wake ulianza Januari 2025.

Alisema moja ya faida kubwa waliyoipata tangu waingie kwenye mfumo wa nishati safi ya kupikia ni kupunguza gharama za kutafuta kuni ambapo maafisa wa magereza walikuwa wakiambatana na wafungwa kutafuta kuni katika maeneo hatarishi ya misitu, pamoja na matumizi makubwa ya mafuta kwenye magari yaliyokuwa yakisomba kuni.








Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...