Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kuwekeza katika sekta ya michezo kwa kujenga miundombinu bora na kuweka mazingira wezeshi kwa maendeleo ya vipaji vya vijana nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Ndugu Gerson Msigwa, wakati wa mapokezi ya Timu ya One Tanzanite Football Academy katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, mara baada ya kurejea kutoka nchini Denmark.
Timu hiyo ya vijana iliitumikia vyema Tanzania kwa kushiriki na kutwaa ubingwa wa Mashindano ya Kimataifa ya DANA CUP, mashindano maarufu kwa kukuza vipaji vya soka la vijana duniani.
“Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa maendeleo ya michezo, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa viwanja bora, vituo vya mafunzo na programu za kukuza vipaji. Tunatoa wito kwa sekta binafsi kushirikiana nasi katika kuendeleza vipaji vya vijana wetu,” amesema Msigwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa One Tanzanite Football Academy, Bw. Agapiti Manday, ameishukuru Serikali kwa namna inavyotambua mchango wa michezo katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Ameeleza kuwa kituo hicho kitaendelea kuwekeza katika mafunzo ya vijana na kuhakikisha Tanzania inaendelea kushiriki katika mashindano ya kimataifa kwa mafanikio.
“Ushindi huu ni matokeo ya kujituma kwa vijana wetu, pamoja na mazingira mazuri ya mafunzo tunayowapa. Tunaiomba Serikali iendelee kuwekeza katika ujenzi wa viwanja bora ili vipaji zaidi viweze kustawi,” amesema Manday.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...