Na.Meleka Kulwa-Dodoma

Katika kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wakulima (Nanenane), ambayo kitaifa yatafanyika mkoani Dodoma, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imetoa mikopo ya riba nafuu yenye thamani ya jumla ya Shilingi Trilioni 1.129 katika kipindi cha miaka kumi kwa lengo la kuwawezesha wakulima kiuchumi.

Akizungumza leo Julai 31,2025 jijini Dodoma na waandishi wa habari kuhusiana na maonyesho hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Frank Nyabundege, amesema benki hiyo imejikita kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuleta mageuzi ya kilimo kwa kumkomboa mkulima wa kawaida kupitia upatikanaji wa mikopo nafuu.

“TADB inaendelea kutekeleza wajibu wake wa msingi wa kuwezesha upatikanaji wa fedha kwa wakulima, kwa masharti rafiki. Lengo letu ni kuona kilimo kinakuwa cha kibiashara na chenye tija kwa maendeleo ya taifa,” amesema Bw. Nyabundege.

Bw. Nyabundege, amesema maonyesho ya mwaka huu yatakuwa ya aina yake kwa kuwa yanaashiria mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta ya kilimo kupitia huduma zinazotolewa na benki hiyo kwa wakulima nchini.

"Rais Samia Suluhu Hassan anaingia madarakani, TADB ilikuwa na mtaji wa shilingi milioni 60, lakini mtaji huo umeongezeka kwa kiasi kubwa hadi kufikia shilingi milioni 442. Aidha, Rais Samia aliweka shilingi trilioni moja Benki Kuu ya Tanzania ili Benki Kuu izikopeshe benki za kibiashara kwa riba nafuu ya asilimia 3, na hatimaye mikopo kwa wakulima ipatikane kwa riba ya chini ya asilimia 10, ikilinganishwa na kiwango cha awali cha asilimia 20 hadi 30."amesema

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli, amesema maonyesho ya mwaka huu yameboreshwa zaidi na yanatarajiwa kutoa elimu muhimu kwa wakulima pamoja na wananchi kuhusu teknolojia, mbinu bora za kilimo na fursa za kiuchumi zilizopo katika sekta ya kilimo.

“Nanenane si tu maonyesho, bali ni jukwaa la elimu, mafunzo, na uhamasishaji kwa wakulima wetu. Tunawakaribisha wadau wote kushiriki,” amesema Bw. Mweli.

Maonyesho ya Nanenane mwaka huu yanatarajiwa kuanza rasmi tarehe 1 Agosti, huku mgeni rasmi akiwa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Maonyesho hayo yatawakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo wakiwemo wakulima, taasisi za kifedha, watafiti, na makampuni ya pembejeo kwa lengo la kubadilishana maarifa na kuonyesha mafanikio yaliyopatikana kupitia mageuzi ya sekta ya kilimo nchini.












Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...