
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo,na Kaimu Balozi wa Uturuki nchini Tanzania, Bw. Ali Goktug IPEK,wakibadilishana Mkataba mara baada ya kusaini Azimio la Kamati ya Pamoja ya Biashara (JTC) kati ya Tanzania na Uturuki hafla iliyofanyika leo Julai 23,2025 jijini jijini Dar es Salaam.
Na.Mwandishi Wetu
SERIKALI ya Tanzania imeweka malengo makubwa ya kibiashara kwa kushirikiana na Uturuki, ikilenga kufikia thamani ya biashara ya Dola za Kimarekani bilioni 1. Hii ni sehemu ya jitihada za kuimarisha uchumi wa nchi kupitia diplomasia ya kiuchumi na kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa za Tanzania katika soko la Uturuki.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kusaini Azimio la Kamati ya Pamoja ya Biashara (JTC) kati ya Tanzania na Uturuki, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo,amesema kuwa ushirikiano huo unalenga kuzalisha bidhaa bora na kukuza sekta ya viwanda, kilimo na madini kwa masoko ya kimataifa.
“Kupitia timu ya wataalamu na ushirikishwaji wa sekta binafsi, tutashirikiana katika biashara kama lango kuu la fursa,” amesema Dkt. Jafo.
Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2024, biashara kati ya Tanzania na Uturuki ilikuwa Dola milioni 284, ambapo Uturuki iliuza bidhaa zenye thamani ya Dola milioni 217 kwa Tanzania, ikionesha fursa kubwa bado hazijatumika kikamilifu.
Waziri Jafo ameeleza kuwa mahusiano ya kidiplomasia na kiuchumi kati ya Tanzania na Uturuki yameimarika kwa kasi, hasa baada ya kufunguliwa kwa balozi za nchi hizo mwaka 2009 na 2017 mtawalia.
Amesema kuwa ziara za viongozi wakuu wa mataifa haya, ikiwemo ile ya Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdoğan nchini Tanzania na ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Uturuki mwaka 2024, zimekuwa kichocheo kikubwa cha ushirikiano huu.
Vilevile,amesema kuwa makampuni ya Kituruki yamekuwa sehemu ya miradi mikubwa ya maendeleo nchini, kama vile ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), ambayo imeleta ajira na fursa mpya kwa Watanzania.
“Makampuni ya Uturuki, hasa kwenye SGR, yameweza kufanya biashara ambayo italeta fursa nyingi kwa wananchi wetu,” amesema Waziri Jafo.
Kaimu Balozi wa Uturuki nchini Tanzania, Bw. Ali Goktug IPEK, ameeleza kuwa JTC ni jukwaa muhimu litakalosaidia kuondoa vikwazo vya kibiashara, kurahisisha michakato ya biashara na kuvutia uwekezaji mpya.
“Kamati ya Pamoja ya Biashara itakuwa jukwaa lenye nguvu la kuondoa vikwazo, kukuza uwekezaji, na kufungua fursa mpya kwa mataifa yote mawili,” ameeleza Balozi Goktug.
Ameongeza kuwa Uturuki imejipanga kushirikiana na Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo miundombinu, kilimo, nishati na teknolojia, huku akisisitiza dhamira ya kuimarisha maendeleo ya pamoja chini ya uongozi wa Rais Erdoğan na Rais Samia.
Kwa ujumla, Tanzania ina matumaini makubwa kuwa ushirikiano huu utafungua ukurasa mpya wa maendeleo ya kiuchumi, ajira na mafanikio kwa wananchi wake.


Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo,akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya hafla ya kusaini Azimio la Kamati ya Pamoja ya Biashara (JTC) kati ya Tanzania na Uturuki iliyofanyika leo Julai 23,2025 jijini Dar es Salaam.

Kaimu Balozi wa Uturuki nchini Tanzania, Bw. Ali Goktug IPEK,wakati wa hafla ya kusaini Azimio la Kamati ya Pamoja ya Biashara (JTC) kati ya Tanzania na Uturuki iliyofanyika leo Julai 23,2025 jijini Dar es Salaam.









Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...