
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) inashiriki katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu kama Sabasaba, kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi sahihi na utunzaji wa dawa na vifaa tiba.
Akizungumza katika banda la TMDA, Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dkt. Adam Fimbo, amesema ushiriki wao katika maonesho hayo ni sehemu ya jukumu lao la kuelimisha jamii kuhusu namna bora ya kuhifadhi dawa, matumizi salama na madhara yanayoweza kujitokeza endapo dawa zitahifadhiwa au kutumika visivyo.
“TMDA ipo kwa ajili ya kulinda afya ya jamii kwa kudhibiti ubora, usalama na ufanisi wa dawa pamoja na vifaa tiba. Tunafanya usajili wa dawa baada ya kufanya tathmini ya kina, tunakagua maeneo ya uzalishaji na uuzaji, na tunafuatilia usalama wa dawa katika soko ili kuhakikisha zinatoa matokeo yaliyokusudiwa,” alisema Dkt. Fimbo.
Aidha, Dkt. Fimbo amekanusha uvumi unaosambaa katika jamii kuwa udhibiti wa bidhaa za Chakula na vipodozi umehamishiwa TMDA amesisitiza kuwa hakuna mabadiliko yoyote rasmi yaliyofanyika kuhusu bidhaa hizo, na kwamba taarifa hizo hazina ukweli.
Maonesho ya Sabasaba mwaka huu yameendelea kuwa jukwaa muhimu kwa taasisi mbalimbali kuonyesha huduma na bidhaa zao huku TMDA ikitumia nafasi hiyo kuwafikia wananchi moja kwa moja kwa njia ya maonyesho, elimu ya ana kwa ana, pamoja na utoaji wa vipeperushi vya mafunzo.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...