NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV

GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, amezitaka taasisi zinazotoa mikopo bila kuwa na leseni ya daraja la pili kuacha mara moja, akisisitiza kuwa ni kosa la kisheria.

Aidha, amewashauri wananchi kuhakikisha wanapata huduma za kifedha kutoka kwa taasisi zilizosajiliwa rasmi.

Wito huo umetolewa leo Julai 1, 2025 Jijini Dar es Salaam, na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba katika uzinduzi wa utaratibu wa usimamizi binafsi kwa taasisi za huduma ndogo za fedha za daraja la pili kati ya BoT na Vyama vya watoa huduma ndogo za fedha.

Tutuba amesema mtu anapokwenda kukopa ni muhimu asome masharti na viwango vya riba.

Aidha amesema kuwa kupitia utaratibu uliozinduliwa, BoT itaendelea kuwa na utekelezaji mzuri wa usimamizi binafsi kwani ni nyenzo muhimu kuufikia malengo ya taifa ya kuboresha huduma jumuishi za kifedha .

Amesema BoT imekuja na mbinu ya kudhibiti mikopo umiza kwa Watanzania kwa kuzitaka taasisi zote ndogo za fedha daraja la pili 2600 kujisajili katika vyama vya Umoja wa watoa huduma ndogo za fedha Tanzania(TAMIU) na Taasisi ya Umoja wa taasisi za Huduma ndogo za fedha(TAMFI) ndani ya miezi sita.

Gavana Tutuba amesema kumekuwepo na ongezeko kubwa la watoa huduma ndogo za fedha nchini hivyo BoT itahakikisha inajenga nidhamu nzuri ya soko kutoa huduma zisizoumiza Watanzania.

Amesema taasisi isiyojisajili hadi Desemba, mwaka huu itanyang’anywa leseni na BoT, lengo likiwa kuhakikisha zinatoa huduma nzuri kwa walaji na kuondoa changamoto kwa jamii.

Pamoja na hayo amesema kuwa kiwango cha upatikanaji wa huduma rasmi za fedha nchini bado kiko chini, kutokana na utafiti uliofanyika mwaka 2023 kiwango kilikuwa asilimia 76.

“Tulijiwekea lengo la kufikia asilimia 85 ifikapo mwaka 2028 lakini kwa kasi na ushirikiano tunaouna tutavuka lengo, kwa uwekezaji uliofanywa na serikali naamini mifumo ya kidigitali imekuwa chachu ya watu kutoa huduma hizo,” Amesema

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Sekta ya Fedha BoT, Sadat Musa amesema hatua hiyo ya kuimarisha mazingira wezeshi kwa taasisi za fedha itakuza uchumi na kuongeza ujumuishi wa huduma za fedha nchini.

Nae Mwenyekiti wa TAMFI, Devotha Minzi, amepongeza mpango huo kama hatua kubwa ya mafanikio kwa sekta ya fedha ndogo, akisema utaongeza kwa kiasi kikubwa ufanisi na uwajibikaji.




























Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...