Karama Kenyunko, Michuzi TV
UPANDE wa mashtaka katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, umepewa hadi Juni 13, 2025, kuhakikisha unamsomea mshtakiwa huyo maelezo ya mashahidi (committal proceedings), ili kesi hiyo iweze kupelekwa Mahakama Kuu kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Franco Kiswaga, alitoa agizo hilo leo, Julai 30, 2025, wakati shauri hilo lilipoitwa kwa ajili ya kutajwa na kusomwa kwa maelezo ya mashahidi pamoja na idadi ya vielelezo vitakavyotumika katika kesi hiyo.

Awali, Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga aliiambia mahakama kuwa hawajawasilisha taarifa ya mashtaka Mahakama Kuu kwa kuwa waliwasilisha maombi ya kutaka kulinda taarifa za mashahidi, ambayo bado hayajatolewa uamuzi.

"Maombi hayo yenye namba 17059/2025 tayari yalisikilizwa Mahakama Kuu, na uamuzi wake unatarajiwa kutolewa Agosti 4, mwaka huu," alieleza Katuga.

Alifafanua kuwa, kwa kuwa maelezo ya mashahidi yanahusiana moja kwa moja na maombi hayo ya ulinzi, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ameshindwa kupeleka taarifa hiyo Mahakama Kuu hadi uamuzi wa maombi hayo utakapojulikana.

Hata hivyo, Lissu alipinga maelezo hayo akisema kuwa tayari mahakama ilishatoa amri kuwa ifikapo Julai 30, 2025 taarifa hiyo iwe imewasilishwa, jambo ambalo halijatekelezwa.

"Tunapoteza muda kwa ahirisho zisizo na msingi. Kama kweli mahakama hii ni huru, basi ikatae ahirisho hili. Kila mara wanakuja bila taarifa, ni matumizi mabaya ya mahakama na dharau kwa amri zako, mheshimiwa," alisema Lissu kwa msisitizo.

Aidha, aliongeza kuwa kukubali kila hoja ya upande wa mashtaka ni sawa na kuhalalisha njama za kunyimwa haki na kukandamiza haki za watu kwa kutumia taasisi za sheria.

Akihitimisha hoja hizo, Hakimu Kiswaga alisema kesi hiyo itaendelea Julai 13, 2025, akieleza kuwa hoja zimekuwa zikijirudia mara kwa mara na kwamba anahitaji muda wa kutafakari kabla ya kutoa uamuzi wa mwisho kuhusu hatua inayofuata.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Lissu anadaiwa kutenda kosa la uhaini Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam. Inadaiwa kuwa alitoa kauli inayochochea uasi kwa kusema:

"Walisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hiyo ndio namna ya kupata mabadiliko... kwa hiyo tunaenda kukinukisha sanasana huu uchaguzi tutaenda kuvuruga kwelikweli, tunaenda kukinukisha vibaya sana."

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...