Katika kuadhimisha miaka 25 ya utoaji huduma nchini, Kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania imeendesha mafunzo kwa mawakala wake zaidi ya 120 kutoka Kanda ya Kati, kwa lengo la kuwawezesha kutambua na kudhibiti uhalifu wa kifedha unaoendelea kuathiri sekta ya huduma za kifedha kwa njia ya mtandao.


Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo yaliyofanyika mkoani Morogoro, Mkuu wa Kanda ya Kati wa Vodacom, Chia Nchimbi, alisema kuwa kampuni hiyo imechukua hatua madhubuti kuhakikisha mawakala wake wanakuwa na uelewa sahihi kuhusu mbinu mpya za kihalifu, namna ya kujikinga, pamoja na kukuza huduma na bidhaa za kampuni hiyo.

"Mafunzo haya ni sehemu ya mkakati wa Vodacom kuhakikisha wateja wetu wananufaika na huduma salama, huku tukiwajengea uwezo mawakala wetu kuwa sehemu ya mapambano dhidi ya uhalifu wa kifedha," alisema Nchimbi.

Kwa upande wake, Nancy Bagaka, Mkuu wa Idara ya M-Pesa Mauzo na Usambazaji Vodacom, alisisitiza kuwa elimu hiyo pia imelenga kuimarisha mbinu bora za usambazaji wa huduma za kifedha, sambamba na kuhimiza matumizi salama ya M-Pesa miongoni mwa wananchi.

Mbali na mawakala, wafanyabiashara wadogo wa huduma za kifedha pia walipewa darasa la namna ya kuepuka mikopo isiyo rafiki inayoweza kuathiri ukuaji wa mitaji yao.

Mkufunzi wa masuala ya fedha binafsi, Edmund Mwijage, aliwataka mawakala kuzingatia nidhamu ya kifedha na kutambua hatari zilizojificha katika miamala ya kila siku.

"Ni muhimu kwa mawakala kufahamu si tu namna ya kuhudumia mteja, bali pia kujua namna ya kulinda mitaji yao dhidi ya udanganyifu wa kimtandao," alisema Mwijage.

Mawakala waliopata mafunzo hao walionyesha kufurahishwa na hatua hiyo, wakisema imeongeza uelewa wao kuhusu namna bora ya kujilinda na kusaidia wateja wao kuwa salama kifedha.

"Kwa kweli tumejifunza mengi, hasa jinsi ya kutambua miamala hatarishi na kujilinda na udanganyifu," alisema Faraja Jeremiah, mmoja wa mawakala walioshiriki.

Maadhimisho hayo ya miaka 25 ya Vodacom yaliambatana na kaulimbiu isemayo “Tupo Nawe Tena, Tena na Tena,” yakihusisha Mawakala Wakuu kutoka mikoa ya Dodoma, Singida na Morogoro, huku lengo kuu likiwa ni kuboresha huduma na usalama wa kifedha nchini.
Mshiriki wakala Richard Malisa akipokea hundi ya fedha  ya kiasi cha Tsh 200,000 kutoka kwa timu ya M-Pesa ya Vodacom baada ya kumaliza mafunzo na maadhimisho ya miaka ya 25 ya kampuni ya Vodacom yaliyofanyika mkoani Morogoro, ambapo mawakala zaidi ya 120 wa huduma za Kifedha kutoka kanda kati ( Dodoma, Morogoro na Singida) walijengewa uwezo wa kutambua na kuthibiti uhalifu wa kifedha sambamba na kuongeza uelewa kuhusu bidhaa na huduma za  Vodacom.









Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...