Na: Calvin Gwabara – Dar es
salaam.
Kamishna wa Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Bi. Amina Talib Ali, amesema Tume hiyo ni
mdau mkubwa katika utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria
(OCPD) hasa katika kuhakikisha sheria zinaandikwa kwa kuzingatia Haki na
Utawala Bora.
Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Bi. Amina Talib Ali akipokea zawadi kutoka kwa Bw. Philemon Mrosso Mwandishi wa Sheria kutoka OCPD Bandani hapo. |
Hayo ameyasema wakati alipotembelea
Banda la OCPD kwenye maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya SabaSaba
yanayoendelea kwenye viwanja vya Mwl. Nyerere Jijini Dar es salaam.
“Moja ya vitu vya msingi THBUB inatakiwa
kuzingatia ni kuhakikisha kuwa Sheria zinazotungwa zinazingatia mikataba ambayo
Tanzania imeridhia kuhusiana na haki za binadamu na utawala bora. Kwa minajili
hiyo, sisi ni wadau wakubwa wa mchakato mzima wa uandishi wa sheria.” Alieleza Kamishna
Ali.
Katika kufafanua ushiriki wa
THBUB katika mchakato mzima wa uandishi wa sheria, alieleza kuwa, kwa mujibu wa
Ibara ya 130 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano na kifungu cha 6 cha Sheria ya
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Sura ya 391, THBUB ina majukumu ya kutoa
mapendekezo kuhusu sheria zilizopo au zinazopendekezwa, kanuni au masharti ya
kiutawala kwa madhumuni ya kuhakikisha uzingatiaji wa misingi ya haki za
binadamu na utawala bora. Aidha, THBUB pia inahamasisha kuridhiwa au kujiunga na
mikataba au makubaliano yanayohusiana na haki za binadamu ikiwa ni Pamoja na
kuratibu sheria za Tanzania ziendane na mikataba hiyo na kufuatilia na
kutathmini uzingatiaji wa haki za binadamu ndani ya Jamhuri ya Muungano,
Serikali au watu wengine.
Aidha Kamishna Ali ameongeza kuwa
Tanzania ni moja kati ya nchi ambazo zimeridhia mikataba mingi ya kimataifa
inayohusu haki za binadamu na utawala bora hivyo katika utekelezaji wa shughuli
zake, lazima ihakikishe haivunji kipengele chochote katika mkataba iliyoiridhia
katika nyanja hizo.
“Naielewa sana kazi nzuri na
kubwa mnayoifanya katika uandishi wa sheria za nchi, na tunatambua mchango wenu
katika kuhakikisha mapendekezo ya kutunga au kurekebisha sheria na sera
zinazoletwa kwenu kwa ajili ya kuzifanya kuwa sheria. Hakika mnafanya kazi
nzuri ya kuzingatia mambo muhimu ya haki za binadamu na utawala bora
zinazingatiwa.” Alieleza Kamishna Ali.
Bw. Philemon Mrosso Mwandishi wa
Sheria kutoka OCPD amemueleza Kamishna makujukumu makuu ya OCPD kuwa ni; kuandika
sheria, kufanya urekebu wa sheria, kufanya ufasili wa sheria pamja na nyaraka
zote za kisheria zinazowasilishwa Bungeni na masuala mengine yote yanayohusiana
na uandishi wa sheria.
Bw. Mrosso alieleza, ili
kuwezesha utekelezaji wenye ufanisi wa majukumu ya Ofisi hiyo, wamekuwa wakitoa
mafunzo ya mara kwa mara kwa waandishi wa sheria na mawakili wa serikali kwa
lengo la kuwajengea uwezo wa kufahamu masuala yote ya msingi wakati wa uandishi
wa sheria.
Akieleza kuhusu kusitishwa
kutumika kwa Toleo la Urekebu wa Sheria la Mwaka 2002 pamoja na matoleo mengine
yote yaliyofuata, Bw. Vincent Masalu mwandishi wa sheria kutoka OCPD amewataka
wadau wa sheria na nchini kutambua kuwa toleo hilo limesitishwa kutumika rasmi
tarehe 1/07/2025 kufuatia tamko rasmi la Mheshimiwa Rais alilolitoa tarehe 24
Aprili 2025 wakati akizindua Toleo la Urekebu wa Sheria la Mwaka 2023.
“Toleo jipya la urekebu la mwaka
2023 lenye jumla ya sheria kuu 446 zilizofanyiwa Urekebu ndilo limeanza
kutumika kuanzia tarehe 1 Julai 2023, hivyo kuanza kutumika kwa Toleo jipya la
mwaka 2023 kunasitisha matumizi ya matoleo yote ya urekebu ya miaka ya nyuma kabla
ya toleo hili jipya la urekebu la mwaka 2023” alifafanua Bw. Masalu.
Aidha, Bw. Masalu alieleza kuwa kwa
kutekeleza amri hiyo ya Mheshimiwa Rais, Sheria zote zilizofanyiwa urekebu
mwaka 2023 tayari zimewekwa katika tovuti ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
nakala mango za sheria hizo zinaendelea kusambazwa katika Wizar ana taasisi zote
za umma, lakini pia nakala nyingine za sheria hizi zinasambazwa na kuuzwa kwa
wananchi wote.
Bw. Masalu amesema juhudi hizi zote
ni katika kuhakikisha kuwa sheria hizi zinawafikia wadau na wananchi ili
kurahisisha upatikanaji wake na kupunguza changamoto ya suala zima la kutumia
sheria ambazo ni vipandevipande vinavyoleta ugumu katika kufanya rejea na hata
upatikanaji haki.
Katika hatua nyingine Bi Mariam
Possi, mwandishi wa sheria, aliwasihi wananchi, wadau na umma kwa ujumla kufika
katika banda la OCPD ili kuweza kupata elimu kuhusiana na mchakato mzima wa
uandishi wa sheria nchini na kupata fursa ya kuona majuzuu ya Toleo la Urekebu
wa Sheria la Mwaka 2023 pamoja na kupata nakala ya machapisho mbalimbali
yanayotumika na Ofisi yetu katika kutekeleza majukumu haya adhimu kwa
mustakabali wan chi yetu.
“Moja kati ya majukumu yetu ni
kutoa elimu kwa umma kuhusiana na mchakato wa uandishi wa sheria. Hivyo tumefungua
milango yetu kwa kuileta Ofisi yetu karibu na wananchi katika maonesho haya ya
kimataifa waweze kuijua na kupata elimu moja kwa moja kutoka kwa waandishi wa
sheria ambao usiku na mchana wanafanya kazi kwa weledi na ufanisi ili
kuhakikisha sheria zinaitikia kauli mbiu yake ya “Sheria Fasaha kwa Utekelezaji
Bora”.” Alisisitiza Bi. Possi.
Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Bi. Amina Talib Ali akizungumzia mahusiano ya kiutendaji yaliyopo kati ya Tume na OCPD. |
Bw. Philemon Mrosso Mwandishi wa Sheria kutoka OCPD akitoa maelezo na ufafanuzi kuhusu majukumu ya Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria kwa Kamishna Ali bandani hapo. |
Bw. Vincent Masalu mwandishi wa sheria kutoka OCPD akiwa ameshikilia moja ya juzuu la Toleo la urekebu wa sheria la mwaka 2023 na kutoa maelezo kwa mwananchi. |
Watumishi wa ofisi ya OCPD wakimkabidhi zawadi Afisa Uchunguzi mwandamizi wa Tume ya haki za binadamu na utawala Bora Bwana Pontian Kitorobombo. |
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...