Na Said Mwishehe,Michuzi TV




MAMLAKA ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA)imewakaribisha wananchi wanaofika katika Maonesho ya Biashara ya 49 ya Kimataifa yanayoendelea Sabasaba jijini Dar es Salaam kufika katika banda lao ili kupata uelewa wa masuala yanayohusu uwekezaji katika masoko ya mitaji.
Akizungumza leo na waandishi wa habari katika Banda la CMSA lililopo katika Jengo la Wizara ya Fedha katika maonesho hayo yanayoendelea Sabasaba Stella Anastaz ambaye ni Afisa Uhusiano na Elimu kwa Umma amesema CMSA imeshiriki Maonesho kwa lengo la kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masoko ya mitaji.
“CMSA ina jukumu la kusimamia Sekta ya Masoko ya Mitaji nchini, na katika msimu huu wa 49 wa maonesho ya kimataifa ya biashara Dar es Salaam tumeshiriki pamoja na watalaam wetu wa soko ambao wanashiriki kwa namna moja au nyingine kuwasaidia wawekezaji".
“Kwahiyo napenda kuchukua fursa hii kuwakaribisha wananchi ambao watapata nafasi ya kuja Sabasaba wasikose kupita banda la CMSA ili waweze kukutana na watalaam wa soko waliobobea katika nyanja mbalimbali za soko ikiwemo uwekezaji katika hisa , uwekezaji kwenye vipande pamoja na uwekezaji katika hati fungani.
“Wananchi watakaofika hapa wanaweza kupata ufahamu wa masuala mbalimbali yanayohusu masoko ya mitaji pamoja na kupata majibu ya maswali yao ndio maana tunawaarifu wananchi waje CMSA kwasababu hapa tumekuja na watalaam wote wa soko.
Amefafanua kuwa watalaam wa masoko wanaotoa elimu na kujibu maswali ya wananchi ni wabobezi na wamepewa leseni na Mamlaka hiyo baada ya kuhitimu kozi maalum ambayo inaendeshwa na Mamlaka.
Watalamu hao kazi yao kubwa ni kutoa ushauri wa wapi uende kuwekeza baada ya kumsikiliza mwekezaji na kujua huyu ni nwekezaji wa namna gani kwasababu kwenye upande wa masoko ya mitaji huu ni uwekezaji wa muda mrefu .
“Kwahiyo akija mtu ambaye anategemea labda aweke leo na baada ya siku mbili tatu atoke inaweza kumletea ukakasi lakini kwa mwekezaji ambaye ana mpango wa muda mrefu akifika hapa ataweza kueleweshwa zaidi.
Wakati huo huo amewaalika wanafunzi ambao wako kwenye vyuo vikuu pamoja na vyuo vingine vya elimu ya juu kufika katika banda la CMSA kwasababu Julai mpaka Agosti mwaka huu wanaprogramu ya shindano la wanafunzi wa elimu ya juu ,ambapo shindano hilo lina lengo la kutoa elimu ya masoko ya mitaji kwa vijana katika sekta ya elimu
“Kwahiyo wakifika hapa wataeleweshwa ni jinsi gani watajisajili na hatimaye kuweza kufanya challenge hiyo.Kwa ambao hawataweza kufika watembelee tovuti ya Mamlaka ambayo ni www.cmsa .go. tz wataweza kukutana na taarifa za ni namna gani wanaweza kujiunga kwenye shindano hili ambapo wakijiunga kwenye shindano hili zawadi mbalimbali zitatolewa .
“Zawadi za fedha pamoja na kutembelea masoko ya mitaji kuona ni namna gani masoko ya mitaji yanafanya kazi na namna gani cmsa inasimamia uwekezaji kwenye masoko ya mitaji,” amesema Anastazi.
Kuhusu usalama wa masoko ya mitaji amesema ni salama kabisa pia ni aina sahihi kabisa ya uwekezaji,kama inavyoeleweka CMSA ni mkono wa Serikali ambao unasimimamia utimilifu wa uwekezaji huo ikiwa pamoja na kuangalia uwiano kati ya wakala wa soko , soko lenyewe na wawekezaji.






Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...