Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jacobs Mwambegele akizungumza wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa watendaji wa uchaguzi mkuu kutoka mikoa ya Shinyanga na Simiyu leo Julai 21, 2025. Mafunzo hayo yamefanyika mkoani Shinyanga.  
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jacobs Mwambegele akizungumza wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa watendaji wa uchaguzi mkuu kutoka mikoa ya Shinyanga na Simiyu leo Julai 21, 2025. Mafunzo hayo yamefanyika mkoani Shinyanga.


Washiriki wa mafunzo hayo ambayo yanawajumuisha waratibu wa uchaguzi, wasimamizi wa uchaguzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo kutoka majimbo yote ya Mikoa ya Shinyanga na Simiyu. 
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume, Ndg. Cyprian Mbugano akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo ambapo pia alitoa mada. 
Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani (Mstaafu) Mbarouk Salim Mbarouk akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo kama hayo kwa Kisiwani Pemba, Zanzibar ambapo amewaasa watendaji hao kufanya kazi kwa kuzingatia Katiba, Sheria, Kanuni, miongozo na maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na yatakayotolewa na Tume.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ndg Adam Mkina ambaye ni Mkurugenzi wa INEC ofisi ya Zanzibar akizungumza jambo. 
Washiriki wa mafunzo hayo ambayo yanawajumuisha waratibu wa uchaguzi, wasimamizi wa uchaguzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo kutoka majimbo yote ya Kisiwani Pemba, Zanzibar.

*******
Na. Mwandishi wetu, Shinyanga
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imewataka watendaji wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kutoa taarifa mapema kwa vyama vya siasa kuhusu utaratibu wa kuwaapisha mawakala.
 
Hayo yamesemwa mkoani Shinyanga leo Julai 21, 2025 na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jacobs Mwambegele wakati akifungua mafunzo kwa watendaji wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi oktoba mwaka huu kwa tarehe itakayotangazwa na Tume.
 
“Wakati wa kuapisha mawakala, toeni taarifa mapema kwa vyama vya siasa kwa mujibu wa sheria, kanuni na maelekezo ya Tume na kuvipatia vyama vya siasa orodha ya vituo vya kupigia kura ili kuviwezesha kupanga mawakala,” amesema Jaji Mwambegele.
 
Amewasisitiza watendaji hao kuhakikisha vifaa vya uchaguzi wanavyopokea kutoka Tume, wanavihakiki, kuvikagua na kuhakikisha vinasambazwa kwenye vituo vyote na kila mkuu wa kituo anapata vifaa vyote vya uchaguzi vinavyohitajika mapema.
 
Amewataka kuhakikisha kuwa siku ya uchaguzi wanaweka utaratibu utakaowezesha kila kituo cha kupigia kura kufunguliwa saa 1:00 kamili asubuhi na kufanya mawasiliano na Tume pale ambapo ushauri utahitajika kuhusiana na masuala ya uchaguzi.
 
Akifungua mafunzo kama hayo Kisiwani Pemba, Zanzibar, Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani (Mstaafu) Mbarouk Salim Mbarouk amewaasa watendaji hao kufanya kazi kwa kuzingatia Katiba, Sheria, Kanuni, miongozo na maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na yatakayotolewa na Tume.
 
 “Jitahidini na mjiepushe kuwa vyanzo vya malalamiko kutoka kwa vyama vya siasa na wadau wa uchaguzi. Hakikisheni mnazingatia ipasavyo Katiba, Sheria, Kanuni, miongozo na maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na yatakayotolewa na Tume,” amesema Jaji Mwambegele.
 
Amewataka kuwashirikisha wadau wa uchaguzi kwenye maeneo wanayopaswa kushirikishwa kwa mujibu wa Katiba, Sheria, Kanuni, miongozo na maelekezo ya Tume.
 
Amewakumbusha kuhusu wajibu wao wa kuhakikisha wanavitambua vituo vya kupigia kura mapema ili kubaini mahitaji maalum ya vituo husika na kuhakikisha kunakuwa na mpangilio mzuri ambao utaruhusu uchaguzi kufanyika kwa utulivu na amani.
 
“Ajira za watendaji wa vituo zizingatie kuajiri watendaji wenye weledi, wanaojitambua, wazalendo, waadilifu na wachapakazi na kuachana na upendeleo kwa ndugu na jamaa ambao hawana sifa za kufanya shughuli za uchaguzi,” amesema Jaji Mbarouk.
 
Mafunzo hayo yanafanyika kwa siku tatu kwenye mikoa mbalimbali nchini kwa siku tatu na yanawajumuisha waratibu wa uchaguzi, wasimamizi wa uchaguzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo.

Tume imeyagawa mafunzo hayo kwenye awamu mbili ambapo awamu hii ya pili inahusisha mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Kusini Pemba, Kaskazini Pemba, Mwanza, Mara, Dar es Salaam, Pwani, Rukwa, Katavi, Manyara, Arusha, Songwe na Mbeya.
 
Awamu ya kwanza ilifanyika tarehe 15 hadi 17 na ilihusisha watendaji kutoka mikoa ya Morogoro, Singida, Dodoma, Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, Mjini Magharibi, Geita, Kagera, Mtwara, Lindi, Tabora, Kigoma, Tanga, Kilimanjaro, Ruvuma, Iringa na Njombe.
Hakimu mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Shinyanga, Mhe. Goodselda Kalumuna akitoa maelezo kabla ya kuwaapisha washiriki hao wa mafunzo kwa watendaji wa Uchagzi Mkuu ambapo aliwaongoza kula kiapo cha kujitoa uanachama na kutunza siri wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao ya Uchaguzi. 


Washiriki wamafunzo kutoka Shinyanga na Simiyu wakila kiapo cha kujitoa uanachama wa vyama vya siasa na kutunza siri. 

Washiriki wamafunzo kutoka Kisiwa cha Pemba, Zanzibar wakila kiapo cha kujitoa uanachama wa vyama vya siasa na kutunza siri. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...