Daktari Bingwa wa maradhi ya kina mama na Uzazi Ummulkulthum Omar


Na Nihifadhi Abdulla, Zanzibar.
WATAALAMU wa afya wameshauri wazazi kuhakikisha wanawachunguza watoto wao mara tu wanapozaliwa, siyo tu kuangalia afya ya jumla, bali pia sehemu zao za siri, ili kubaini mapema matatizo ya kiafya yanayoweza kuathiri maisha yao baadaye.

Ushauri huu umetolewa kufuatia matukio kadhaa yanayoripotiwa ya baadhi ya watoto kuzaliwa na matatizo kama korodani moja au matatizo ya kuwa na viashiria vya jinsia mbili, hali ambayo kitaalamu hujulikana kama Disorders of Sex Development (DSD).

Daktari Bingwa wa maradhi ya kina mama na Uzazi wa Hospitali ya Mnazimmoja Ummulkulthum Omar amesema mara nyingi wazazi wanapozaliwa mtoto wa kiume hushangilia na kuona kila kitu kipo sawa, lakini hawachunguzi kwa makini hali ya vyumba vya siri vya watoto wao. “Unakuta mtoto amezaliwa ana korodani moja au viashiria vingine vinavyoleta mashaka, lakini watu husema acha akue kwanza. Kumbe tatizo linaweza kuwa kubwa zaidi kuliko wanavyodhani,” amesema Dk. Ummu.

Amefafanua kwamba baadhi ya watoto huzaliwa wakiwa na tatizo la korodani moja, ambalo kitaalamu huitwa undescended testis, ambapo korodani moja inashindwa kushuka kwenye sehemu yake ya kawaida.

Shirika la Afya Duniani (WHO) katika ripoti yao ya Global Health Observatory ya mwaka 2022, ikionyesha kwamba kati ya kila watoto 1,000 wanaozaliwa, angalau 4 hadi 5 wanazaliwa na matatizo ya sehemu za siri vinavyohusiana na jinsia mbili au korodani moja, ingawa kiwango hiki kinaweza kutofautiana kutoka nchi moja hadi nyingine.

Kwa mujibu wa WHO, Disorders of Sex Development (DSD) siyo nadra kama jamii inavyodhani, na takwimu zinaonesha kwamba hali hii hutokea kwa wastani wa mtoto mmoja kati ya kila watoto 4,500 hadi 5,500 wanaozaliwa duniani kote.

Katika ripoti ya Disorders of Sex Development 2023 WHO imesisitiza kwamba “utambuzi wa mapema” ni jambo muhimu kwa sababu matibabu yanapochelewa yanaweza kuleta madhara makubwa kiafya, kisaikolojia na kijamii kwa watoto hawa. “Ni muhimu kila mtoto anayezaliwa kuchunguzwa sehemu zake za siri, siyo kwa sababu tu ya afya ya mwili, bali pia kwa sababu ya ustawi wake wa baadae

Zainab Suleiman, mkaazi wa Jumbi wilaya ya Kati Zanzibar mama wa mtoto aliyezaliwa na korodani moja, ameeleza jinsi alivyopitia changamoto hiyo alijifungua mtoto wa kiume na kufurahia kama wazazi wengine, lakini baadaye aligundua kuna tofauti. “Nilipojifungua niliona mtoto wangu ana korodani moja tu. Wauguzi walisema labda nyingine itashuka baada ya muda. Tulingoja, lakini haikushuka. nilipokwenda tena hospitali madaktari wakanieleza kuwa mtoto ana tatizo ,” amesema Zainab.

Zainab amesema wakati anapata taarifa hizo, moyo wake ulimuuma sana, kwani hakuwahi kufikiria kwamba mtoto wake angekumbwa na hali kama hiyo. “Nilikuwa sijui kabisa haya mambo. nilidhani mtoto wa kiume lazima awe na korodani mbili. Niliona aibu na sikuwa tayari kumwambia mtu,” amesema Zainab

Dk ummulkulthum amesema matatizo kama haya yakigundulika mapema, huwa yana nafasi kubwa ya kutibiwa kwa njia ya upasuaji mdogo au matibabu ya homoni, hivyo kumwepusha mtoto na matatizo makubwa ya kiafya na kisaikolojia anapokuwa mtu mzima.

Amesema iwapo matatizo haya hayataangaliwa mapema, kuna hatari ya kupelekea mtoto kupata saratani kwenye korodani iliyofichika au matatizo ya utambulisho wa jinsia. “Hii siyo hali ya kumcheka mtu. ni jambo la kitabibu linalohitaji huruma, elimu na msaada wa jamii,” amesema Daktari

Baada ya vipimo zaidi, madaktari walimhakikishia Zainab kuwa mtoto wake hana chembechembe za jinsia nyingine na kwamba ni wa kiume, ingawa angehitaji ufuatiliaji wa kitabibu ili kuhakikisha afya yake inaendelea vizuri. “Waliniambia mtoto wangu anaweza kuishi maisha ya kawaida kabisa, lakini lazima awe anakaguliwa mara kwa mara. Namshukuru Mungu na madaktari,” amesema Zainab kwa tabasamu dogo la matumaini.

Kwa upande wake, Zaina Abdalla Mzee, Afisa wa Mradi wa Afya ya Uzazi na Haki za Afya ya Uzazi (SRHR) kutoka TAMWA Zanzibar, amesema taasisi yao imeona kuna haja kubwa ya kutoa elimu kuhusu matatizo ya Afya kwa mama na mtoto kwa vile Zanzibar bado uelewa ni mdogo kuhusu hali hii. “Tunataka jamii ijue kwamba matatizo yeyote kimbilio ni Hospital,” amesema Zaina kwa msisitizo.

Zaina amesema mradi huo unakusudia kutoa elimu katika kliniki za wajawazito na pia kupitia vyombo vya habari ili kufikisha ujumbe kwa watu wengi zaidi. Huku akieleza kuwa wanashirikiana na madaktari ili kutoa elimu sahihi na kuondoa aibu iliyopo kwenye jamii kuhusu matatizo haya. “Tunataka kila mzazi ajue kwamba mtoto anapozaliwa lazima achunguzwe, si kuangalia uso na mikono pekee. Hata sehemu zake za siri lazima ili yapatikane matibabu ya mapema,” amesema Zaina.

Kwa mujibu wa WHO, watoto wenye matatizo kama korodani moja au jinsia mbili wana nafasi kubwa ya kuishi maisha yenye afya bora endapo watapata matibabu mapema na ushauri wa kitaalamu. Shirika hilo limeeleza kuwa kuchelewa kugundua matatizo hayo huongeza uwezekano wa mtoto kupata saratani, matatizo ya uzazi au matatizo ya kisaikolojia yanayoweza kumfanya mtoto ajione hana thamani katika jamii. “Mapema ndiyo tiba,”

Zainab Suleiman anasema changamoto kubwa aliyopitia ilikuwa maneno ya watu na woga wa kutengwa kwenye jamii kuna wakati alikuwa anajilaumu mwenyewe akidhani labda kuna jambo baya alilofanya wakati wa ujauzito. “Nilijilaumu sana. nilidhani labda kuna kitu nilikula au nilikosea. lakini madaktari waliniambia si kosa langu. ni hali ya kimaumbile,” amesema Zainab huku akifuta machozi.

Zainab kwa sasa ana faraja baada ya mtoto wake kuendelea vizuri kiafya na amepata matumaini kuwa ataishi maisha ya kawaida sambamba na kuwaomba wazazi wenzake kutokuwa na aibu kupeleka watoto hospitalini mara wanapoona dalili za hali isiyo ya kawaida. “Mimi nimejifunza. bora aibu kidogo kuliko matatizo makubwa baadaye. wazazi wenzangu tusikae kimya,” amesema Zainab.

Kwa sasa, wataalamu wa afya na taasisi kama TAMWA Zanzibar pamoja na WHO wanaendelea kutoa wito kwa jamii kupeleka watoto hospitalini mara tu wanapozaliwa ili kuhakikisha wanachunguzwa na kugundulika mapema iwapo wana matatizo yoyote. Dk. Ummy amesisitiza kwamba wazazi waache kusema eti mtoto akikua matatizo yatapona yenyewe. “Tuwe na utamaduni wa uchunguzi wa mapema. Hii ni afya ya mtoto wetu na maisha yake ya baadaye,” amemalizia Daktari kwa kutilia mkazo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...