
Makubaliano haya yanatazamwa kama hatua kubwa ya mageuzi katika kukuza ujumuishaji wa kidijitali na kupanua upatikanaji wa huduma za mawasiliano za kuaminika barani Afrika.
Ushirikiano wa awali utahusisha mgawanyo wa mtandao wa mkongo na minara ya mawasiliano, hatua itakayoharakisha upanuzi wa huduma za kidijitali katika masoko husika, kuongeza upatikanaji wa huduma kwa wateja, kupunguza gharama za miundombinu kwa watoa huduma, na kuongeza kasi ya kufikisha huduma sokoni.
Kwa kutumia miundombinu iliyopo, Airtel na Vodacom wanalenga kuboresha muunganisho, kuongeza kasi ya intaneti na kutoa huduma bora zaidi, hatua hii itaboresha uzoefu wa wateja na pia kusaidia kutoa huduma za kidijitali kwa idadi kubwa zaidi ya watu, hususan maeneo yaliyo na huduma hafifu, hivyo kusaidia kuziba pengo la kidijitali barani Afrika.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Vodacom Group, Shameel Joosub, alisema; "Kutoa muunganisho ili kuwawezesha watu ndiyo kiini cha mkakati wetu, ushirikiano wetu na Airtel Africa ni hatua chanya kuelekea katika kujenga mustakabali wa kidijitali endelevu, jumuishi na wenye muunganisho barani Afrika, kupitia mgawanyo wa miundombinu, tunaweza kutoa huduma nafuu kwa watu wengi zaidi, kwa haraka, na kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma katika zama hizi za kidijitali."
Bwana Joosub aliongeza kuwa makubaliano haya yana nafasi kubwa ya kupunguza pengo la kidijitali na kuwawezesha watu na jamii kupitia kidijitali, sambamba na lengo la Vodacom la kuunganisha wateja milioni 260 kufikia mwaka 2030.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Airtel Africa, Sunil Taldar, alisema; "Ushirikiano huu unaendana na dhamira yetu ya kuhakikisha mtandao wetu unapatikana hata katika maeneo ya mbali kabisa, kushirikiana na Vodacom kutafungua fursa kubwa zaidi za kidijitali na kifedha ambazo zitabadilisha maisha ya wateja wetu huku tukizingatia matakwa yote ya kisheria."
Bwana Taldar alisisitiza kuwa hata kama makampuni haya ni washindani kibiashara, kushirikiana katika miundombinu muhimu ni jambo la lazima ili kujenga mitandao imara yenye uwezo mkubwa wa kusaidia teknolojia mpya na mahitaji yanayoongezeka ya huduma zinazotumia data.
Aliongeza kuwa kuharakisha upanuzi wa muunganisho wa mkongo wa baharini ni nyenzo muhimu katika kuendeleza teknolojia za 4G na 5G barani Afrika, ili kutoa huduma zenye kasi ya juu, ucheleweshaji mdogo (low latency) na uaminifu unaohitajika kwa matumizi ya kisasa ya kidijitali.
Makubaliano haya yanatoa fursa kwa pande zote mbili kuboresha zaidi utendaji wa mitandao, kupanua upeo wa huduma, na kuongeza upatikanaji wa huduma za simu, intaneti ya nyumbani, na huduma za kifedha, kwa kutumia mtandao mpana zaidi barani Afrika.
Vodacom Group’s chief executive officer Shameel JoosubAirtel Africa’s chief executive officer Sunil Taldar
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...