Kibamba, Agosti 27, 2025 – Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kibamba kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhe. Angellah Kairuki, amerudisha rasmi fomu ya uteuzi kwa Tume Huru ya Uchaguzi (INEC), hatua muhimu kuelekea kuteuliwa rasmi kugombea ubunge katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.
Mhe. Kairuki aliwasili katika ofisi za INEC akiambatana na mgombea ubunge wa Jimbo la Ubungo kupitia CCM, Mhe. Kitila Mkumbo, na kusindikizwa na mamia ya wanachama wa CCM, madereva wa bodaboda, bajaji pamoja na wafanyabiashara wadogo maarufu kama Mama Ntilie, waliokuwa wakionesha mshikamano na kumuunga mkono.
Akizungumza mara baada ya kurejesha fomu, Mhe. Kairuki alieleza dhamira yake ya dhati kuwatumikia wananchi wa Jimbo la Kibamba kwa uadilifu na bidii kubwa.
"Ari ninayo, lakini pia uwezo wa kuwatumikia wananchi wa Kibamba ninao. Nimejipanga kuhakikisha tunaleta maendeleo ya kweli katika kila kata ya jimbo letu,” alisema.
Mhe. Kairuki aliongeza kuwa kampeni zake zitajikita kwenye hoja na sera, sambamba na kueleza kwa kina mafanikio ya Serikali ya CCM kupitia utekelezaji wa ilani ya chama hicho.
“Tutatumia kampeni hizi kuwaeleza wananchi nini tumefanya na nini tunatarajia kufanya ili kuboresha maisha yao. Lengo letu ni kuwaletea furaha, faraja na maendeleo endelevu.”
Hatua ya kurejesha fomu ni ishara ya kujipanga kwa CCM kuendelea kulitumikia Taifa kwa kuzingatia misingi ya haki, maendeleo na ustawi wa wananchi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...