-Utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko ameupongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kuendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa vitendo.

Ametoa pongezi hizo Jijini Dodoma Agosti 21, 2025 wakati wa Hafla ya uhamasishaji matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa wadau wanaochoma nyama katika Mnada wa Msalato.

"Nawapongeza Watendaji REA na Wizara ya Nishati kwa kutekeleza maelekezo ya kuhakikisha wananchi wanaelimishwa, wanahamasishwa na wanawezeshwa kutumia Nishati Safi ya Kupikia," alisema Mhe. Dkt. Biteko.

Alisema ziara yake mnadani hapo ililenga kuhamasisha umuhimu wa kutumia Nishati Safi ya Kupikia kwa Wachoma nyama na Mama Lishe wanaofanya shughuli zao katika mnada huo.

Alibainisha kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alielekeza ifikapo mwaka 2034; 80% ya Watanzania wawe wanatumia Nishati Safi ya Kupikia.

"Tulianza katika taasisi zinazohudumia zaidi ya watu 100; nafurahi kueleza hapa kwamba magereza yote nchini na taasisi zingine wameanza kutumia Nishati Safi ya Kupikia," alisema

Aidha, aliielekeza REA kuhakikisha majiko makubwa yaliyoboreshwa yanawafikia Wachoma Nyama katika mnada huo ili kupunguza matumizi makubwa ya kuni na mkaa.

Sambamba na hilo, alitoa maelekezo kwa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kuhakikisha Mkaa Mbadala unapatikana katika eneo la mnada ili wananchi walioanza kutumia mkaa huo kutorudi nyuma.

Alisema lengo ni kuhakikisha minada yote nchini inaanza kutumia Nishati Safi ya Kupikia na kwamba mnada huo wa Msalato utakuwa mfano wa kuigwa na minada mingine.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini, Mha. Hassan Saidy alimuahidi Mhe. Dkt. Biteko kuwa REA itatekeleza kwa weledi maelekezo yake.

Mha. Saidy alielezea hatua mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na REA ikiwemo kuhamasisha, kutoa elimu na kuwezesha upatikanaji wa bidhaa mbalimbali za Nishati Safi ya Kupikia.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...