Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma
MGOABEA urais kupitia Chama Cha Makini, Coaster Kibonde, amechukua fomu ya kugombea nafasi hiyo katika ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), huku akiahidi iwapo watanzania watamchagua kila kijana wa Kitanzania mwenye umri wa kuanzia miaka 21 atapewa ekari tano za ardhi kwa ajili ya shughuli za kilimo.
Kibonde anakuwa mgombea wa nne kuchukua fomu akitanguliwa na Rais Samia Suluhu Hassan na Dkt Emmanuel Nchimbi (CCM) Kunje Ngombare Mwiru na Chumu Abdallah Juma ,Chama cha Wakulima (AAFP) na Hassan Almas na Ally Hassan (NRA).
Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu, Kibonde ambaye aliambatana na mgombea mwenza wake, Bi. Azza Haji Suleiman, amesema kuwa serikali yake inalenga kuwahamasisha vijana kuingia kwenye kilimo cha kisasa chenye tija, badala ya kutegemea kilimo cha jadi ambacho hakina manufaa ya kudumu.
“Tutafanya kilimo cha umwagiliaji ili kuachana kabisa na kilimo cha kutegemea mvua ambacho ni kilimo cha umasikini. Maana ya Chama Makini ni Maarifa,kila kijana tutampatia ekari 5 kwa ajili ya kulima kwa kutumia matrekta, amesema Kibonde.
Amevitaja vipaumbele vya Chama hicho ni elimu, Kilimo na Afya lengo likiwa ni kuhakikisha wanaondoa umaskini kwa watanzania.
Kibonde alisisitiza kuwa elimu itakuwa kipaumbele cha kwanza katika utawala wake huku akiweka mkazo mkubwa katika kuhakikisha kila kijana wa Kitanzania anapata elimu ya kiwango cha kimataifa.
“Ukimnyima Mtanzania elimu ni sawa na kumfunga gerezani maisha. Sisi tutalivalia njuga suala la elimu tutahakikisha elimu inayopatikana duniani kote inamfikia kijana wa Kitanzania,” amesema Mgombea huyo
Kwa upande wa afya, Kibonde amesema serikali yake itaweka mkazo mkubwa katika kuimarisha huduma za afya nchini kwa kujenga hospitali katika kila kata pamoja na kuzipatia vifaa tiba vya kisasa.
“Ukimnyima Mtanzania afya ni sawa na kumhukumu kifo tutahakikisha tunakuwa na wataalamu wa kutosha kwa sababu tutawekeza sana katika elimu ya afya,” alisema.
Alitangaza pia kuwa serikali yake itaanzisha bima ya afya kwa wote itakayojulikana kama MakiniCare, ambayo italenga kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za afya bila ubaguzi.
Vyama vingine vinavyotarajiwa kuchukua fomu leo ni National League (NLD) na United People Democratic (UPDP).
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...