Na Said Mwishehe, Michuzi TV
WIZARA ya Maliasili na Utalii imezindua Mpango Mkakati wa kitaifa wa Maendeleo na usimamizi wa mikoko nchini huku Waziri wa Wizara hiyo Dk.Pindi Chana akitoa maelekezo kwa mamlaka mbalimbali kuhakikisha zinalinda na kuhifadhi mikoko.
Akizungumza leo Agosti 5,2025 jijini Dar es Salaam wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mikoko Duniani pamoja na uzinduzi wa Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Maendeleo ya usimamizi wa Mikoko Waziri Dk.Pindi Chana amesisitiza umuhimu wa kuendelea kulinda hifadhi za mikoko.
“Taasisi za utafiti hakikisheni mnafanya tafiti za kisayansi na zenye mlengo wa matumizi ya teknolojia zitazotuwezesha kuhifadhi na kuwa na matumizi endelevu ya misitu ya mikoko.
“TFS hakikisheni mnashirikiana na mamlaka nyingine kulinda na kuhifadhi maeneo ya hifadhi za mikoko, hakikisheni mnashirikiana na wadau kuanzisha miradi itakayohifadhi misitu hii pamoja na kuwawezesha wananchi wanaopakana na maeneo ya hifadhi ya mikoko.
“Wizara ya Maliasili na Utalii shirikianeni na Mamlaka nyingine ili kuhakikisha kuwa maeneo ya hifadhi za mikoko yanatumiwa kama sehemu ya kivutio cha utalii.”
Aidha Dk.Pindi Chana amemshukuru Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ambaye ni Mhifadhi namba moja kwa maono na maelekezo yake ya kuhakikisha kuwa wanaendelea na kuhifadhi maliasili zetu.
“Tanzania ni mojawapo ya nchi zenye eneo kubwa la misitu ya mikoko yenye takriban hekta 158,100 ambayo imesambaa katika Wilaya 14 za Pwani, kutoka Mtwara kusini hadi Tanga kaskazini na katika visiwa vya Unguja, Pemba na Mafia.
“Hifadhi za Mikoko si tu ina umuhimu mkubwa kwa Tanzania, bali pia ni sehemu ya mfumo ikolojia wa kimataifa wa Bahari ya Hindi. Mikoko inachangia katika afya ya Bahari; uhifadhi wa mazalia ya Samaki; kuhifadhi fukwe dhidi ya mmomonyoko wa ardhi
“Pia kuhifadhi kaboni; kuchuja taka; na kudhibiti mabadiliko ya tabianchi katika ukanda mzima wa bahari. Kwa hiyo, kulinda hifadhi za mikoko ni kulinda maisha ya watu na viumbe hai.”
Pamoja na na faida mbalimbali zinazopatikana amesema bado hifadhi za mikoko zimekuwa zikikabiliwa na changamoto kadhaa.Bado kumekuwa na uharibifu mkubwa wa mikoko kwa ajili ya kuanzisha shughuli za kibinadamu.
Pia amesema uko uvunaji haramu wa mazao ya mikoko na uchafuzi wa mazingira katika maeneo ya hifadhi za mikoko pamoja na ujenzi holela katika maeneo ya hifadhi hizi. Hali hiyo imeendelea kuathiri ikolojia ya hifadhi ya mikoko na hivyo tumeanza kuona matokeo hasi katika maeoneo yetu ya Pwani.
Amesema zipo jitihada za kuhifadhi misitu ya mikoko zinazofanywa na Serikali,wadau wa maendeleo na Sekta binafsi. Miongoni mwa jitihada hizo ni uwepo wa mkakati maalum wa Usimamizi na Uendelezaji wa Rasilimali za Mikoko wa mwaka 2025-2035 ambayo ameizindua leo.
Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS)Profesa Dos Santos Silayo amesema mikoko ni miti au vichaka maalum vinavyoota katika maeneo ya pwani yenye maji ya chumvi au mchanganyiko wa chumvi na baridi, hasa katika mabonde ya mito, delta, na maeneo ya bahari yenye mawimbi madogo.
Ameongeza miti hiyo imezoea mazingira magumu yenye chumvi nyingi, ardhi tambarare na huchipua katika matope au mchanga wa pwani. Ikologia hiyo ya mikoko inapatikana katika takriban nchi 123 duniani ambazo zipo katika mabara manne: Afrika, Asia, Amerika, na Oceania.
“Kutokana na umuhimu wake kimazingira na kiuchumi, Shirika la UNESCO lilipendekeza kuwa Julai 26 ya kila mwaka iwe Siku ya Kimataifa ya Mikoko. Katika kuhakikisha kuwa siku hii inaadhimishwa kikamilifu Tanzania tulianza kufanya shughuli mbalimbali zinazohusiana na uhifadhi wa miti ya Mikoko.
“Miongoni mwa kazi zilizofanyika tangu tarehe 26 Julai ni kupanda takriban miche ya mikoko 5000 na kufanya usafi kwenye mwambao wa bahari.Pia leo tunazindua Mkakati huu pamoja na kufanya Kongamano la Kisayansi na mijadala mbambali.”
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...