Songea-Ruvuma.
Mathew Ngalimanayo ameanza rasmi safari yake ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu kwa kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya Udiwani wa Kata ya Mjini Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akipokea fomu hiyo katika ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Mjini leo, Ngalimanayo amesema kuwa dhamira yake kuu ni kuhakikisha anawaletea wananchi maendeleo ya kweli yanayotekelezeka kwa vitendo, si kwa ahadi zisizo na utekelezaji.
Ametoa wito kwa wakazi wa kata hiyo kutupilia mbali siasa za majukwaani zisizo na tija na badala yake waelekeze nguvu katika kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Amelitaja suala la kudumisha amani na mshikamano kuwa ni msingi muhimu wa mafanikio ya maendeleo endelevu, akieleza kuwa ushirikiano kati ya viongozi na wananchi ni silaha muhimu katika kufanikisha malengo ya kijamii na kiuchumi.
Pia amewahamasisha wananchi wa Kata ya Mjini kuendelea kuiamini na kuiunga mkono CCM kwa kuwa ni chama chenye dira, misingi na sera makini za kuwaletea maendeleo Watanzania.
Amesisitiza umuhimu wa ushiriki mkubwa wa wapiga kura katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba, akihimiza ushindi wa kishindo kwa CCM.
Wanachama wa CCM walijitokeza kwa idadi kubwa kumsindikiza Ngalimanayo kuchukua fomu hiyo, safari ya maandamano ya amani ilianzia katika ofisi za CCM mtaa wa Zanzibar kuelekea kwenye ofisi za kata, ikiwa ni ishara ya mshikamano na imani waliyonayo kwake kuelekea uchaguzi huo.
Mwenyekiti wa CCM Kata ya Mjini, Rotali Nikata, amesema chama kimejipanga kuhakikisha kinashinda kwa kishindo katika nafasi zote za udiwani, ubunge na urais na amewataka wanachama kushikamana kuhakikisha lengo hilo linafanikiwa.
Naye Katibu wa CCM wa kata hiyo, Mikaela Komba, amewataka wanachama kuwa mabalozi wa chama kwa kufanya kazi nzuri na kushiriki kikamilifu kwenye mchakato wa uchaguzi, ili kuhakikisha masilahi ya kata na chama yanalindwa na kuendelezwa.
Kwa kauli moja, viongozi na wanachama wa CCM wameonyesha matumaini makubwa kwa Ngalimanayo na kumuahidi ushirikiano wa karibu katika safari yake ya kisiasa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...