Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Chemba

WAKULIMA sasa ni neema tele kwao! Hivyo ndivyo unavyoweza kuelezea baada ya Mgombea Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM)Dk.Samia Suluhu Hassan kuahidi kufanya mageuzi makubwa katika sekta hiyo ikiwemo mpango wa kununua matrekta Milioni 10 katika miaka mitano ijayo ili kuwawezesha wakulima kukodisha trekta kwa nusu bei ya ile inayokodishwa na watu binafsi.

Mbali ya matrekta pia Rais Samia ameahidi kuendelea kununua vifaa na zana za kilimo ambazo zitasambazwa katika vituo vyote vinavyojihusisha na kilimo nchini lengo likiwa kuwarahisishia wakulima kupata zana  hizo kwa urahisi na gharama nafuu.

Akizungumza na maelfu ya wananchi wa Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma leo Agosti 31,2024 katika mkutano wake wa kampeni Rais Samia amesema anatambua juhudi ambazo Serikali imezifanya katika sekta ya kilimo lakini miaka mitano ijayo kuna mambo makubwa zaidi yanakwenda kufanyika katika sekta ya kilimo nchini.

Rais Dk.Samia amesema iwapo wananchi watamchagua katika kipindi cha miaka mitano ijayo mpango wa Serikali yake itanunua matrekta milioni 10 katika kipindi cha miaka mitano na kusisitiza matrekta hayo yatakodishwa kwa wakulima nusu ya bei wanatakayotozwa na watu binafsi wanapolimiwa kwa kila ekari moja.

"Tunampango wa kununua matrekta milioni 10 ifikapo 2030, tutanunua na zana zingine ili tuanzishe vituo katika kanda ambavyo pembejeo zote za kilimo zitapatikana. 

“Lengo ni kumpunguzia mkulima adha ya kukodi vifaa na zana za kilimo kwa watu binafsi ambao kwa ekari moja wanalimiwa hadi sh. 80,000 ambazo wamenza kushusha kufikia sh. 40,000 baada ya serikali kuanza kuweka vituo hivyo,”amesema Rais Samia alipokuwa akitoa ahadi hiyo kwa wananchi wa Chemba wilayani Kondoa.

Hata hivyo amefafanua kwa bei yeyote ambayo sekta binafsi itawatoza wakulima, serikali itatoza nusu ya bei hiyo huku akieleza kwamba  ili hayo yatimie basi ni vema wakamchagua kwa nafasi ya Rais sambamba na wabunge na madiwani wa CCM ambayo kauli yao inasema Kazi na Utu Tunasonga mbele.”Naomba mfanye hivyo kaipigieni kura CCM katika mafiga matatu ili safari yetu iendelee."

Akieleza kwa kina kuhusu zana za kilimo, mgombea Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Serikali  imeanza kuunda kanda za zana za kilimo ambapo kwa Dodoma itaangaliwa eneo gani litafaa kuwekwa kanda hiyo.

Amesema kwa Kondoa na Chemba wataangalia uwezekano wapi kanda hiyo iwekwe lakini suala la zana za kilimo, mara ya kwanza walianza na matrekta 500 na pawatila 800.

“Serikali itaanzisha kongani za viwanda kila wilaya, hivyo kwa wilaya hiyo utafiti utafanyika kubaini shughuli zipi kubwa zinazofaa kuanzishwa kongani za viwanda.Lile ombi la kongani za viwanda tutaangalia ndani ya Chemba kuna kitu gani cha uchumi.

“Hicho ndicho tutakachokiwekea kongani ya viwanda. Kama ni mazao ya kilimo ni mazao gani, kama ni mifugo tutaweka kongani ya mifugo. Kwa hiyo inategemea Chemba kuna kitu gani cha uchumi lakini tunajipanga kuanzisha kongani za wilaya za viwanda," amesema Rais Dk.Samia.














Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...